DRC-RWANDA

DRC yakosoa uamuzi wa Rwanda kuwafutia uraia watu wake walio katika nchi jirani

rfi

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC imekosoa hatua iliyotangazwa na mamlaka za nchi ya Rwanda kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu, itawafutia uraia wananchi wake wanaohifadhiwa kwenye makambi ya wakimbizi katika nchi jirani iwapo hawatawarejea nchini humo kwa hiari yao.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari jijini Goma, Gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Julein Paluku amesema Rwanda haiwajibiki kuchukua hatua kama hiyo wakati raia wake wengi walipokelewa na mataifa kadhaa yaliyo jirani.

Aidha Gavana Julien Paluku amethibitisha kuwa kwenye mkutano uliomalizika mjini Pretoria Aprili 18, serikali ya DRC ilidhihirisha kuwa Jimbo la Kivu ya Kaskazini ndilo lenye idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Rwanda na kwamba walikubaliana na serikali ya Rwanda kuondoa Mpango wake wa kufuta utambulisho wa mkimbizi kwa wakimbizi wa Rwanda.

Waziri wa mambo ya ndani wa DRC Muyej Mangaz amethibitisha Taifa lake la Congo linawahifadhi wakimbizi takribani laki moja na ishirini elfu ambao wengi baadhi yao walikimbilia Congo tangu pale yalipofanyika mauaji ya halaiki nchini Rwanda mnamo mwaka wa 1994.

Rwanda imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa usalama wa ndani umekamilika hivyo hakuna haja kwa raia wake kuendelea kuishi nje ya nchi katika makambi ya wakimbizi.