SOMALIA

Mwanahabari mwingine auawa baada ya kupigwa risasi nchini Somalia

Mwandishi mwingine wa habari Mohamed Ibrahim Rageh ameuawa mjini Mogadishu nchini Somalia baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana na kufikisha idadi ya wanahabari waliouawa nchini humo mwaka huu kufikia wanne.

Matangazo ya kibiashara

Chama cha kitaifa cha waandishi wa habari nchini humo NUSOJ kimelaani mauaji ya Rageh aliyekuwa anafanya kazi katika idhaa ya taifa ya runinga na redio Mogadishu nchini humo.

Taarifa ya NUSOJ imebainisha kuwa Rageh alishambuliwa siku ya jumapili wakati alipokuwa anarejea nyumbani kutoka kazini.

Mashambulizi na mauaji ya waandishi wa habari yameendelea kuwa tishio katika tasnia ya habari nchini humo, takribani waandishi 18 waliauwa katika kipindi cha mwaka 2012.

Mapema mwaka huu, serikali ya Somalia ilitangaza dau ya dola za Marekani elfu hamsini kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa taarifa sahihi juu ya wahusika wa mauaji ya waandishi wa habari.