DR Congo

Kiongozi wa Kikosi cha Jeshi linalotarajiwa kuingia Mashariki mwa Congo afanya ziara Mashariki mwa nchi hiyo

Kiongozi wa Waasi wa M23, Betrand Bisimwa
Kiongozi wa Waasi wa M23, Betrand Bisimwa Photo AFP / Isaac Kasamani

Kiongozi wa Kikosi cha kijeshi cha Umoja wa Mataifa kinachotarajiwa kuingia Mashariki mwa nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo yuko mjini Goma kwa ajili ya kufanya ziara ya kiupelelezi.

Matangazo ya kibiashara

Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa Tanzania amefanya ziara mjini humo sambamba na mji wa Sake kutathimini ni eneo gani ambalo vikosi vitawasili, Msemaji wa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO, Alexandre Essome.
 

Jenerali huyo aliongoza jopo la Wataalam katika maandalizi ya kuundwa kwa Kikosi cha kimataifa cha kulinda amani, hatua ambayo baadae ilibadilishwa na kuwa kikosi cha uvamizi kwa ajili ya kupambana na makundi ya uasi.
 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliazimia tarehe 28 mwezi March kuunda kikosi kitakachokuwa na jukumu la kupambana na Makundi ya uasi Mashariki mwa DRC hususan, Waasi wa M23.
 

MONUSCO ilipatiwa jukumu la kufanya Operesheni kuhakikisha inalinda Raia, kuzuia Makundi ya Waasi kushamiri na kunyang'anya silaha Makundi hayo.
Afrika kusini, Tanzania na Malawi inatarajiwa kutoa Wanajeshi wake na kuunda Jeshi moja lenye Watu 3,069.
 

M23 kwa upande wake imeapa kulipa kisasi iwapo itashambuliwa na Vikosi hivyo ,likitaka Afrika kusini na Tanzania kuachana na mpango wa kupeleka Vikosi Mashariki mwa Congo.