DR Congo

Mazungumzo ya kupata Suluhu ya Congo yakwama huko Kampala

Kiongozi wa Waasi wa M23, Betrand Bisimwa
Kiongozi wa Waasi wa M23, Betrand Bisimwa Photo AFP / Isaac Kasamani

Mazungumzo ya kusaka amani ya kudumu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC yamekwama kwa mara nyingine huku wajumbe kutoka serikali ya Kinshasa na Kundi la Waasi la M23 wanaoshiriki kwenye mchakato huo wakirudi nyumbani.

Matangazo ya kibiashara

Kukwama kwa mazungumzo haya kumepokelewa kwa mitazamo tofauti na wananchi ambao wanahisi hakuna umakini kutoka pande zote mbili zinazoshiriki mazungumzo hayo.

Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Kinshasa huko Uganda Francois Mwamba amesema wao wanasubiri maelekezo kutoka kwa mpatanishi wa mgogoro huo Cryspus Kiyonga ili kuendelea pale walipoishia.

Tangu kuanza kwa mazungumzo ya kusaka amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC huku Kampala kumekuwa na vikwazo vingi na kuchangia kushindikana kupigwa hatua na kufikiwa suluhu ya kweli.

Katika hatua nyingine Mjumbe maalum wa jumuia ya nchi za ukanda wa Maziwa Makuu kutoka Umoja wa Mataifa, ambaye ni Rais wa zamani wa Ireland na Mwanaharakati Mary Robinson juma lijalo atafanya ziara yake ya kwanza katika eneo la ukanda wa maziwa makuu.

Ziara ya Bibi Robinson ambayo itamfikisha nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Uganda, Burundi na Afrika kusini itaanza siku ya jumatatu na kumalizika tarehe 5 mwezi May kwa kutembelea Makao makuu ya Umoja wa Afrika AU nchini Ethiopia.

Robinson anajukumu la kuongoza jitihada za kisiasa za kumaliza mgogoro katika ukanda huo.

Wakati wa ziara yake, Robinson ataanzisha mazungumzo na Viongozi na Maafisa kutoka nchi za ukanda huo ambazo hivi karibuni zilitia saini mpango wa ushirikiano na amani kwa ajili ya nchi ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ili kumaliza mapigano Mashariki ya DRC.
 

Mjumbe huyu anatarajiwa kuwasili Kinshasa ambapo atakutana na Rais Joseph Kabila , Waziri wa mambo ya nje Raymond Tshibanda na Viongozi wa Majeshi ya MONUSCO.