SUDANI

Waasi Sudan sasa watangaza kulenga jimbo la Kordofan Kaskazini

Reuters/Mohamed Nureldin Abdallah

Waasi wa Sudan wametangaza kuwa rasmi kuwa wanalilenga jimbo la Kordofan Kaskazini kama njia ya kujihami na kujilinda dhidi ya majeshi ya serikali huku wakijipanga kusonga mbele. 

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo inakuja huku Bunge la nchi hiyo likiwa limetana mwishoni mwa juma kujadili mashambulizi ya mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo hilo la Kordofan Kaskazini ambalo limekuwa tulivu kwa kipindi kirefu.

Eneo hilo limekuwa tulivu tangu kuanza kwa mgogoro wa Drfur lakini siku ya jumamosi iliyopita muungano wa waasi ulishambulia eneo hilo ambalo halina ulinzi imara kwa sababu ya utulivu.
 

Msemaji wa waasi SPLM-N, Arnu Ngutulu Lodi amesema kuwa jimbo sasa ni miongoni mwa maeneo yanalengwa na waasi hao kwani eneo ambalo limekuwa na vita ni Kordofan Kusini na si kaskazini.
 

Waasi wa SRF ambao ni washirika wakubwa wa SPLM-N wamesema walishambulia Umm Rawaba ambao ni mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Kordofan Kaskazini na maeneo mengine upande wa Kordofan Kusini kama njia ya kupenya na kuingia katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
 

Waasi hao wamesema wanataka kuingia Khartoum ili kuundoa madarakani utawala wa Rais Omar Al Bashar uliodumu kwa miaka 24 na hatimaye kuwakomboa watu wa Sudan.
 

Katika hatua nyingine Serikali hivi karibuni ilitoa wito wa kufanya mazungumzo na waasi lakini wito huo unaonekana kupuuzwa na waasi hao hali ambayo inaongeza utata zaidi katika mgogoro huo.