AFRIKA KUSINI

Idadi ya askari wa Afrika Kusini waliokufa Jamhuri ya Afrika ya Kati yafikia 14

RFI

Wizara ya Ulinzi nchini Afrika Kusini imetangaza kifo cha mwanajeshi wake aliyejeruhiwa katika mapigano kule nchini jamuhuri ya Afrika ya kati machi 23, wakati waasi wa kundi la Seleka walipoiteka nchi na kumgo'a rais Francois Bozize madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi la Afrika kusini Jenerali Xolani Mabanga amesema Mwanajeshi huyo amefikisha idadi ya wanajeshi 14 ambao waliuawa katika mapigano hayo miezi kadhaa iliopita.

Hata hivyo duru kutoka nchini Afrika kusini zaarifu kuwa mwanajeshi huyo alikuwa amepata nafuu na kuruhusiwa kurejea nyumbani wakati akipata matibabu, na ilitakiwa afanyiwe uchunguzi kwa mara nyingine tena siku ya Ijumaa juma hili.

Wanajeshi 13 walitangazwa kupoteza maisha huku wengine 27 wakijeruhiwa wakati wa mapambano na waasi wa muungano wakundi la Seleka jijini Bangui Marchi 23 siku moja tu baada ya rais Francois Bozize kulazimika kuitoroka nchi.

Tangu hapo Afrika kusini iliamua kuyaondowa majeshi yake yaliyokuwepo nchini Jamujhuri ya Afrika ya Kati kwa lengo la kutowa mafunzo kwa wanajeshi wa Jamuhuri ya Afrika ya kati.

Vifo vya wanajeshi hao vilizua mjadala mkubwa nchini Afrika kusini ambapo Upinzani unadai kuwa wanajeshi hao walitolewa kafara na kusisitiza kuwa chama tawala nchinI humo kilikuwa kinafanya biashara ya alimasi nchini jamuhuri ya Afrika ya kati.