JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Serikali ya Bangui yaundiwa mfuko maalumu wa kuisaidia katika kipindi cha mpito

AFP PHOTO / SIA KAMBOU

Majirani wa Jamhuri ya Afrika ya kati wameazimia kuunda mfuko maalumu utakaoisaidia serikali ya Bangui kujiimarisha katika kipindi hiki cha mpito baada ya utawala mpya wa Seleka kuingia madarakani. Azimio hilo limefikiwa katika mkutano wa kimataifa wa majirani wa nchi hiyo uliofanyika nchini Congo Brazaville siku ya ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika mkutano huo Rais wa mpito wa Afrika ya kati Michel Djotodia ameahidi fedha zitakazopatikana katika mfuko huo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kufadhili mchakato wa uchaguzi ambao utafanyika mwaka 2014.

Aidha wadau wa mkutano huo wametoa wito kwa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati ECCAS, Umoja wa Afrika AU na wahisani mbalimbali kuchangia mfuko huo ili kuiwezesha nchi hiyo kwa sasa.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ambaye alikuwepo katika mkutano huo ametoa wito kwa nchi hizo kuendelea kuweka mikakati thabiti ya kulisaidia Taifa hilo ili liweze kupata suluhu ya kisiasa na kuepusha madhara zaidi katika siku za usoni.

Zuma amesema kuzorota kwa usalama katika Taifa hilo kunapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee ili kuepukana na matokeo ambayo huenda yakaathiri nchi nyingine katika ukanda huo na hata katika bara la Afrika.

Jamhuri ya Afrika ya kati ambayo kwa sasa inaongozwa na muungano wa waasi wa Seleka iliingia madarakani machi 24 mwaka huu baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Francois Bozize.