Wanamgambo waliozingira Wizara nchini Libya watangaza mpango wa kuipindua Serikali ya Waziri Mkuu Zeidan
Imechapishwa:
Wanamgambo waliojihami kwa silaha nchini Libya ambao wanaendelea kushikilia Wizara za Sheria na Mambo ya Nje wameibuka na madai mapya na kwa sasa wanataka serikali yote ambayo ipo madarakani kutangaza kujiuzulu kutokana na kushindwa kushughulikia madai yao.
Watu hao ambao wamejihami kwa silaha nzito za kivita walikuwa wanadai kuondolewa kwa Viongozi wote waliokuwa wanahudumu chini ya Utawala wa Kiongozi wa zamani Marehemu Kanali Muammar Gaddafi.
Kilio cha watu hao wenye silaha kimesikilizwa na Bunge na hatimaye kupitisha Sheria ya kuwaondoa mamlakani Viongozi wote waliokuwa kwenye Utawala wa Marehemu Kanali Gaddafi na wanaendelea kushika nyadhifa mbalimbali.
Kiongozi wa Wanamgambo hao Osama Kaabar amesema wao wanachokitaka kwa sasa ni kuona Viongozi wote wa zamani wanaondoka kwenye serikali ili Utawala mpya uanze kazi ya kuongoza nchi hiyo.
Kaabar ameongeza kuwa wataendelea na mapambano yao hadi pale ambapo Waziri Mkuu Ali Zeidan naye atakapoondoka madarakani kwa kile ambacho wanadai ameshindwa kutekeleza malengo ya mapinduzi yaliyofanywa.
Kiongozi wa Wanamgambo hao Kaabar amesema wamefurahishwa na hatua ya Bunge kupitisha sheria hiyo mpya lakini huo ni mwanzo tu wa kutekelezwa kile ambacho kipo kwenye sheria na ndiyo maana wao wanataka hatua zaidi zichukuliwe.
Kaabar ameweka bayana nia yao ni kuiangusha serikali ya Waziri Mkuu Zeidan ambayo imekosa mwelekeo uliosababisha kuangushwa kwa serikali ya Marehemu Kanali Gaddafi hivyo wao watasimamia hilo.
Tamko hilo linakuwa ni kitisho kikubwa kwa serikali ya Waziri Mkuu Zeidan ambayo kwa zaidi ya majuma mawili imeshuhudia wizara zake mbili zikizingirwa na wanamgambo hao waliojihami kwa silaha na kulazimisha kukamwa kwa shughuli kutokana na kufungwa kwake.