LIBYA

Waziri wa Ulinzi wa Libya Al Barghathi ajiuzulu huku Wanamgambo wakiendelea kutishia kuiangusha Serikali

Waziri wa Ulinzi aliyetangaza kujiuzulu nchini Libya Mohammed al-Barghathi
Waziri wa Ulinzi aliyetangaza kujiuzulu nchini Libya Mohammed al-Barghathi

Hofu ya kisiasa imeendelea kuitikisa Serikali ya Libya baada ya Waziri wa Ulinzi nchini humo Mohammed al-Barghathi kutangaza kujiuzulu ikiwa ni siku moja tangu Wanamgambo wanaoshikilia Wizara ya Sheria na ile ya Mambo ya Nje kutangaza mkakati wao wa kuiangusha serikali iliyopo madarakani. Waziri Al Barghathi amefikia uamuzi huo kutokana na hali tete inayoendelea kuikumba serikali ya Waziri Mkuu Ali Zeidan iliyomatatani kuangushwa na Wanamgambo wanaomiliki silaha za kivita na wenye mkakati wa kuangusha serikali yake.

Matangazo ya kibiashara

Kujiuzulu kwake kumehusishwa na hatua ya Bunge nchini Libya kupitisha sheria ya kuwashinikiza wale wote ambao walifanyakazi chini ya Utawala wa Marehemu Kanali Muammar Gaddafi kuachia nyadhifa zao mara moja.

Bunge lilipitisha sheria hiyo ikiwa ni kujibu shinikizo la Wanamgambo hao ambao wamekuwa wakishinikiza kuondolewa madarakani kwa Viongozi wote waliohudumu chini ya Uongozi wa Marehemu Kanali Gaddafi.

Barghathi alikuwa miongoni mwa Viongozi chini ya Utawala wa Marehemu Kanali Gaddafi na ameonekana kuanza kutekeleza kile ambacho kinatajwa kwenye sheria hiyo inayoanza kufanya kazi katika kipindi cha mwezi mmoja tangu kupitishwa kwake.

Haya yanakuja huku wanamgambo hao wakiendelea kushikilia Wizara hizo mbili kwa zaidi ya majuma mawili huku wakija madai mapya sasa ya kutaka kuiangusha serikali kwa kile ilichosema imeshindwa kufanya kazi zake.

Serikali ya Waziri Mkuu Zeidan imeingia matatani baada ya kujikuta ikiingia kwenye mtego wa kuwapa vyeo Viongozi waliohudumu chini ya Utawala wa Marehemu Kanali Gaddafi kitu ambacho ni kinyume na makubaliano ya kufanyika kwa mapinduzi.

Kiongozi wa Wanamgambo hao wanaomiliki silaha nzito Osama Kaabar amesema hawatokubali kuona Serikali ya Waziri Mkuu Zeidan ikikiuka makubaliano ya kufanyika kwa mapinduzi nchini Libya.

Kaabar amesema watahakikisha wanaiangusha serikali hiyo na kuunda serikali mpya ambayo itakuwa inaheshimu makubaliano ya kufanyika kwa mapinduzi ya kuiangusha serikali ya Marehemu Kanali Muamar Gaddafi.