MALI-UFARANSA

Jeshi la Mali laanzisha oparesheni za kuyadhibiti makundi ya Kiislamu

REUTERS/Adama Diarra

Jeshi la Mali limeanzisha operesheni zake katika maeneo yanayodaiwa kuwa ngome madhubuti za makundi ya Kiislamu hasa kwenye Mji wa Kidal unaotajwa kuwa sehemu ya wapiganaji wa Kundi la MNLA. Jeshi hilo limejiapiza kuhakikisha linawateketeza wapiganaji wote ambao wameendelea kuwa kero katika jitihada za kuimarisha usalama wa maeneo hayo ya kaskazini.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametoa wito kwa mamlaka za nchini humo kuhakikisha wanaelekeza nguvu zaidi katika mji wa Kidal ambao umekuwa ukikumbwa na matukio ya uhalifu yanayoendeshwa na makundi ya wapiganaji.

Oparesheni hizi zinakuja wakati kumeendelea kutolewa shinikizo la kufanyika kwa uchaguzi nchini humo ili kuuleta madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wote kwa njia ya kidemokrasia.

Juma lililopita Rais Francois Hollande alihimiza kuwa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Julai kuendeshwa kwa usawa na demokrasia katika maeneo yote ya nchi hiyo licha ya hofu ya kukosekana kwa usalama katika eneo la kaskazini.

Jeshi la mali kwa kushirikiana na Vikosi kutoka mataifa mengine limeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha linayatokomeza kabisa Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanashikilia eneo la Kaskazini tangu kufanyika kwa mapinduzi ya kuiangusha Serikali ya Rais Amadou Toumani Toure.