MADAGASCAR

Rais wa Madagascar agoma kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina.
Rais wa Madagascar Andry Rajoelina. AFP/Stephane De Sakutin

Rais wa visiwa vya Madagascar Andry Rajoelina amekataa wito wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC uliomtaka kutowania tena Urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Julai. 

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kupitisha vyombo vya habari jana Jumatatu, Rajoelina amesema huu si wakati wa kutafuta matatizo zaidi katika taifa hilo bali wananchi ndio wanapaswa kuamua nani anayefaa kuwa rais wa Madagascar.

Juma lililopita SADC ilimtaka kiongozi huyo wa mpito kujitoa katika kinyang'anyiro cha urais ili kuepusha machafuko katika visiwa hivyo vilivyopo katika bahari ya Hindi.

Madagascar imekuwa katika mtikisiko wa kisiasa tangu Rajoelina aingie madarakani mwaka 2009 baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Marc Ravalomanana, SADC imekuwa ikiwasihi mahasimu hao wawili kujiweka kando na kinyang'anyiro cha urais.