LIBYA

Watu 15 wapoteza maisha na wengine zaidi ya 30 wajeruhiwa katika shambulio la bomu nchini Libya

Wananchi wakishuhudia uharibifu baada ya shambulio la bomu
Wananchi wakishuhudia uharibifu baada ya shambulio la bomu euronews

Watu kumi na watano wamepoteza maisha na wengine zaidi ya thelathini wamejeruhiwa nchini Libya katika Jiji la Benghazi baada ya kutekelezwa shambulizi la bomu la kujitoa mhanga karibu kabisa na jengo la Hospital ya Al Jala. 

Matangazo ya kibiashara

Naibu waziri wa mambo ya ndani Abdullah Massoud ndiye amethibitisha idadi hiyo ya vifo huku akisisitiza kuwa hiyo ni idadi ya awali na kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka ambapo tayari kidole cha lawama kimeanza kuelekezwa kwa wapiganaji wanaomuunga mkono marehemu Kanali Muammar Gaddafi.

Shambulizi hilo baya linakuja kipindi hiki ambacho kumekuwa na hali ya taharuki ya usalama nchini Libya ambapo vituo vinne vya polisi tayari vimeshambuliwa mjini Benghaz hivi karibuni viwili vikiwa vimeshambuliwa Ijumaa iliyopita na vingine viwili vikishambuliwa siku ya Jumapili.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limelaani vikali shambulio hilo la Benghaz huku wajumbe wa baraza hilo wakitilia mkazo wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Libya kufanikisha mageuzi ya kupata demokrasia ya amani na yakudumu.