MALI

Rais wa mpito wa Mali asema uchaguzi lazima ufanyike licha ya changamoto zilizopo

Rais wa Serikali ya Mpito ya Mali, Dioncounda Traore
Rais wa Serikali ya Mpito ya Mali, Dioncounda Traore maliweb.net

Rais wa Mali Dioncunda Traore ameahidi uchaguzi mkuu utafanyika kama ulivyopangwa mwezi Julai licha ya uwepo wa vikwazo kadhaa vinavyowakabili kauli inayokuja huku mataifa wahisani yakikutana kuangalia namna ya kulisaidia Taifa hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Rais Traore amesema uchaguzi utafanyika mwishoni mwa mwezi Julai ikiwa ni hatua ya kumaliza muda wa serikali ya mpito iliyokuwa na jukumu la kuhakikisha hali inatengemaa.

Mkutano wa kuisaidia nchi ya Mali umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya EU ambapo rais wa Burkina Faso Blaise Compaore ameweka wazi lengo la mkutano huo kuwa ni kulisaidia taifa hilo kujiimarisha.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya EU Jose Manuel Barroso ambaye ni sehemu ya waandaaji wa mkutano huo kwa upande wake amekiri wazi kuwa hali ya kisiasa nchini Mali imeimarika kwa kiasi kikubwa.

Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikifanya kila linalowezekana katika kuhakikisha hali ya usalama inaimarika nchini Mali baada ya taifa hilo kupitia kipindi cha mpito cha mabadiliko ya uongozi.