Afrika Kusini-DRC

Wanajeshi wa Afrika Kusini wajifua kabla ya kuelekea Mashariki mwa DRC

Wanajeshi wa Afrika Kusini wakijifua
Wanajeshi wa Afrika Kusini wakijifua timeslive.co.za

Wanajeshi wa Afrika Kusini wanaojiandaa kuungana na kikosi cha Umoja wa Mataifa UN Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wameendelea na mafunzo kwa ajili ya jukumu hilo wakati huu kukiwa na taarifa za jeshi la nchi hiyo kukabiliwa na uhaba wa vifaa na fedha.  

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Luteni Generali V.R Masondo amewathibitishia waandishi wa habari kuwa vikosi vyake vitakavyoelekea DRC vinapata mafunzo maalumu toka kwa wenzao ambao walishiriki katika kikosi kilichotoka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwezi Machi mwaka huu ambapo wanajeshi wa Afrika Kusini 14 waliuawa katika mapambano hayo yaliyomuondoa aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya kati Francois Bozize.

Masondo amesema bajeti ya kiasi cha dola bilioni 1.1 kwa jeshi la Afrika kusini haitoshi kukidhi mahitaji yote na amekiri kuwa wanajeshi wake wanaoelekea Congo wamejiandaa vizuri licha ya changamoto zinazowakabili.

Umoja wa Mataifa ulithibitisha kuwasili kwa kikosi cha kwanza cha wanajeshi mia moja toka Tanzania Mashariki mwa DRC katika harakati za kutokomeza makundi ya waasi, wanajeshi wapatao elfu tatu wanatarajiwa kushiriki katika oparesheni hiyo.