Mali-Maurtania

Msemaji wa kundi la Ansar Dine ajisalimisha Mauritania

Mkuu wa operesheni za kundi la kigaidi lenye uhusiano na kundi la Al Qaeda nchini Mali Senda Ould Boumama amejisalimisha nchini Maurtania leo Jumatatu taarifa kutoka vyanzo vya usalama vimethibitisha. 

Msemaji wa Ansar Dine Senda Ould Boumama
Msemaji wa Ansar Dine Senda Ould Boumama nord-mali.com
Matangazo ya kibiashara

Boumama ambaye ni msemaji wa kundi la Ansar Dine alijisalimisha kwenye vikosi vya kijeshi vya Maurtania mpakani mwa nchi hiyo karibu na Kusini Magharibi mwa mji wa Bassiknou siku ya Jumamosi jioni chanzo hicho kimeeleza bila ya kutoa maelezo zaidi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la kujitegemea nchini Maurtania ANI, Boumama Ould alihamishwa mwishoni mwa juma na kupelekwa kwenye mji mkuu Nouakchott ambako polisi wanaendelea kumhoji.

Awali Boumama alionesha nia ya kujisalimisha na kupewa kinga ya kukabiliana na mashataka nchini mwake Maurtania alipozungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la ANI mnamo April 17.

Kujisalimisha kwake itaonekana kuwa pigo zaidi kwa Ansar Dine miezi minne baada ya Ufaransa kuongoza operesheni ya kijeshi kuuondosha kundi hilo na makundi mengine ya wapiganaji wa Kiislam kutoka katika miji waliyokuwa wanadhibiti kaskazini mwa Mali mwaka jana.