Waasi wa M23 wakabiliana na wanajeshi wa serikali Kaskazini mwa Goma
Waasi wa kundi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wamepigana na wanajeshi wa serikali Kaskazini mwa mji wa Goma leo Jumatatu mji ambao waasi waliudhibiti mnamo mwezi Disemba.
Imechapishwa:
Msemaji wa kundi la M23 Amani Kabasha amesema kuwa mapigano yametokea umbali wa Kilomita 12 Kaskazini mwa Goma, huku msemaji wa majeshi ya serikali ya DRC Kanali Olivier Hamuli akithibitisha kutokea kwa mapigano hayo leo asubuhi ingawa hakueleza ikiwa kuna maafa yaliyojitokeza.
Hapo jana hali ya wasiwasi iliripotiwa kutanda katika maeneo ya mpakani mwa DRC na Rwanda na maeneo kadhaa katika jimbo la Kivu ya Kaskazini baada ya Mashirika ya kiraia kutoa ripoti kuwa waasi hao wa M23 wanatishia kuuteka upya mji wa Goma.
Waasi wa M23 wameendelea kuwa tishio kwa usalama Mashariki mwa DRC kutokana na kuendesha vitisho na mapigano huku wakitishia kushambulia vikosi vya umoja wa mataifa vitakavyopelekwa nchini humo kupambana na makundi ya uasi.