DRC

Jeshi la serikali ya DRC lafanikiwa kurejesha hali ya usalama mjini Mutaho

Jeshi la serikali Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC limesema limefanikiwa kurejesha utulivu katika mji wa Mutaho uliopo kwenye umbali wa kilomita takribani 10 na Jiji la Goma, baada ya kuibuka mapigano makali baina yao na kundi la waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo. 

Wanajeshi wa serikali ya DRC
Wanajeshi wa serikali ya DRC alissaeverett.com
Matangazo ya kibiashara

Watu wa maeneo hayo walishtushwa vikali na milio ya risase ikifutiwa na mizinga iliorushwa kutoka pande zote mbili. Jeshi la Serikali lilitumia mashambulizi ya anga kuwazuia wapiganaji hao kusonga mbele.

Tangu majuma kadhaa kulikuwa na uvumi uliotanda kuhusu wapiganaji wa M23 kujiandaa kuuteka tena mji wa Goma

Mapigano hayo yamesababisha watu zaidi ya elfu mbili kuyahama makaazi yao na kukimbilia katika kambi ya Mugunga, eneo la Magharibi mwa Jiji la Goma. Hakuna taarifa yoyote iliotolewa kuhusu maafa kutoka pande zote mbili aidha majeruhi.

Wakaazi wa maeneo hayo wamesema hali ya wasiwasi inazidi kutanda katika kila maeneo na hata katika Jiji la Goma, huku viongozi wakuu wa serikali pamoja na maafisa wa jeshi wakizidi kuwatolea wito raia kuwa watulivu.

Akizungumza na RFI Kiswahili naibu gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini Felly Rutaichirwa amesema kwamba tangu majuma kadhaa waasi wa M23 wamekuwa wakiongeza vikosi vyao kwenye ngome zao pembeni na mji wa Goma, hali iliopelekea majeshi ya Serikali kujiweka sawa kwa lolote ambalo linaweza kuibuka.

Gavana huyo amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuwa na matumaini kw ajeshi, lakini pia kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa huku wakiendeleza shughuli zao za kila siku bila kuwa na hofu yoyote, kwani majeshi ya serikali yanashguhulikia swala la usalama kama ipasavyo.

Upande wao waasi wa kundi la M23 wamethibitisha kuwa hawana nia yoyote ya kuuteka mji wa Goma bali kinachotakiwa wakati huu ni mazungumzo yatakayoleta amani badala ya kutumia njia za kijeshi na nguvu katika kutatua mzozo huo.

Msemaji wa kisiasa wa kundi hilo, Rene Abandi amesema lengo lao ni kutia mbele mazungumzo ya kisiasa na sio kuendeleza vita,  lakini amesema, hawatoendelea kuvumilia uvamizi unaendeshwa na majeshi ya serikali ya FARDC, kwakuwa hawataki tena vita hivyo visababishe kuuteka tena mji wa Goma.

Hayo yanajiri wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akisubiriwa  kuwasili Jijini Goma, Mashariki mwa nchi hiyo kutathmini hali ya usalama katika eneo hilo lenye utajiri wa madini na ambalo mzozo wa kivita inaibuka mara kadhaa.