Serikali ya Kenya yasema haina wasiwasi ikiwa rais Obama hatazuru taifa hilo
Imechapishwa:
Serikali ya Kenya imesema haina kinyongo na rais wa Marekani Barak Obama ambaye anatarajia kuzuru mataifa ya Afrika mwezi ujao huku akiiondoa Kenya miongoni mwa nchi atakazo zitembelea, na kukanusha kuwa hiyo inatokana na viongozi wake kukabiliwa na mashata dhidi ya ubinadamu.
Obama anatarajia kuanza ziara yake ya kwanza barani Afrika mwishoni mwa mwezi Juni, ambapo atatembelea nchi za Senegal, Tanzania na Afrika Kusini, huku ratiba yake ikiwa haioneshi kama atazuru Kenya ambako baba yake alizaliwa.
Msemaji wa serikali ya Kenya Muthui Kariuki ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa Marekani kama ilivyo Kenya ni taifa huru na rais wake anayo haki ya kidemokrasia kutembelea kokote apendako.
Aidha Muthui ameongeza kuwa Kenya inaendelea na agenda yake ya maendeleo na kwamba taifa hilo linaendelea kuwa sehemu ya Muungano wa Mataifa na kwamba hawana hofu kwamba Obama hatazuru taifa hilo.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais William Ruto, waliochaguliwa mwezi Machi, wote wawili wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) mjini The Hague kwa madai ya kushiriki kwao katika kuchochea vurugu zilizosababisha mauaji baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008.