AFRIKA KUSINI-RIADHA-PISTORIUS

Picha za tukio la mauaji ya mchumba wa mwanariadha wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius zavuja nchini Uingereza

Mwanariadha mwenye ulemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius akiwa mahakamani mapema mwaka huu alipopandishwa kwa mara ya kwanza kusomewa mashtaka yake
Mwanariadha mwenye ulemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius akiwa mahakamani mapema mwaka huu alipopandishwa kwa mara ya kwanza kusomewa mashtaka yake Reuters / Sibeko

Picha mnato zinazoonesha damu kwenye choo cha mwanariadha wa Afrika Kusini mwenye ulemavu Oscar Pistorius zimeripotiwa kuvuja kwenye mitandao ya nchini Uingereza kuonesha tukio la kupigwa risasi kwa mchumba wake.

Matangazo ya kibiashara

Picha hizo mnato zinavujishwa ikiwa zimebaki siku chache kabla ya mwanariadha huyo kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine kuanza kusikiliza kesi ya mauaji inayomkabili.

Picha hizo zinaonesha damu zikiwa zimetapakaa ndani ya choo cha mwanariadha huyo huku sehemu ya ukuta jirani na kikalio cha choo kukionekana matundu mawili ya risasi ambazo zilitumika.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26 mwezi February mwaka huu aliiambia mahakama ya mjini Johanesburg kuwa alimpiga risasi mchumba wake, Reeva Steenkamp baada ya kumdhania kuwa ni mvamizi.

Uchunguzi wa awali wa polisi unaonesha kuwa kuna ukweli kuwa huenda mwanaridha huyo wakati akifyatua risasi hizo alikuwa akitumia miguu yake ya bandia nje ya bafu alimokuwemo mchumba wake.

Kesi ya mauaji dhidi ya mwanariadha huyo imevuta hisia za mashabiki wa mwanamitindo Steenkamp pamoja na mwanariadha huyo huku baadhi wakiwa na maoni tofauti kuhusu namna ambavyo tukio hilo limetekelezwa.