EAC

Serikali za Afrika Mashariki kuwasilisha bajeti zao pamoja

Mawaziri wa fedha katika mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  wanawasilisha bajeti ya makadirio ya fedha za serikali zao ya mwaka 2013/2014 leo Alhamisi  kueleza kiwango cha fedha kilichotengwa kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mataifa yao.

Matangazo ya kibiashara

Bajeti katika mataifa hayo kwa miaka kadhaa sasa imekuwa ikisomwa  siku moja ili kuimarisha zaidi umoja wa jumuiya hiyo ambayo inalenga kuwa na muungano wa kisiasa katika siku zijazo.

Wananchi wa Afrika Mashariki wanasubiri kuona ikiwa bajeti hizo zitagusa maisha yao ya kawaida na kuimarisha maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

Kenya ambayo inaongoza kiuchumi katika kanda hiyo, bajeti yake  inawasilishwa wakati kukiwa na mgawanyiko kati ya bunge la taifa na lile la Senate kutokana na mabunge hayo mawili kupitisha miswada tofauti  kuhusu kiwango cha fedha kinachohitajika kwa maendeleo.

Maseneta nchini humo wanawasilisha kesi katika Mahakama ya juu kutaka ufafanuzi zaidi ikiwa ni sahihi kwa bunge la taifa  kupunguza mapendekezo ya kugawanywa kwa fedha katika serikali za Kauti, mswada uliotiwa sahihi na rais Uhuru Kenyatta.

Ni mara ya kwanza kwa serikali ya rais Uhuru Kenyatta kuwasilisha bajeti yake kwa bunge na wananchi wa taifa hilo miezi michache baada ya kuchaguliwa rais na inakadiriwa kuwa bajeti hiyo huenda ikawa ya Matrilioni ya Shilingi za Kenya.

Wakenya wengi wanahofia kuwa bajeti ya mwaka itakuwa upande wao kutoka na mgawanyiko wa bunge la Senate na kilio kikubwa cha serikali kuwa ina madeni mengi.

Nchini Tanzania, wachambuzi wa maswala ya uchumi wanasema kuwa bejeti ya mwaka huu itakuwa mtihani mkubwa kwa rais Jakaya  Kikwete kutokana na wananchi wake kuendelea kuiomba serikali kupunguza bei ya bidhaa muhimu ili kupunguza kupanda kwa maisha.

Bejeti ya Tanzania inatarajiwa kuwa ya Shilingi Trilioni 17 na miongoni mwa maswala nyeti yatakayopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni pamoja na upatikanaji wa umeme, kuboresha bandari, maji, elimu ujasiriamali pamoja na kilimo.

Nchini Uganda, hali ni kama hiyo na wananchi wanamsubiri Waziri Maria Kiwanuka kuwasilisha bajeti hiyo ambayo inatarajiwa kuongeza kodi kwa bidhaa muhimu kama pombe na sigara kama njia yaa kubana matumzi ya fedha.

Serikali ya Kampala mwaka wa fedha iliyopita imekuwa ikikumbana na hali ngumu ya kifedha baada ya wahisani kutoka mataifa ya Ulaya kusitisha msaada wao kwa nchi hiyo kwa madai ya kuwepo kwa kashfa za ufisadi na fedha hizo kutumiwa vibaya.

Nchini Rwanda Waziri wa fedha Claver Gatete, anatarajiwa kutangaza ongezeko la bajeti ya mwaka huu kutoka Franca Trilioni 1 nkta 4 hadi Franca Trilioni 1 nukta 6.

Bajeti hiyo inatarajiwa kuangazia maendeleo vijijini pamoja na kujenga miradi ya maendeleo likiwemo bwawa la kuzalisha umeme la Nyabarongo.

Nchini Burundi wananchi nchini humo pia wanasubiri ikiwa bajeti ya mwaka huu itasaidia kuimarisha maisha yao hasa baada ya wafanyibiashara wengi kupoteza biashara zao kutokana na kuteketea kwa soko kuu jijini Bunjumbura mapema mwaka huu.