MISRI-MAANDAMANO-MAREKANI

Marekani yawaonya raia wake kujiepusha na machafuko yanayoshika kasi nchini Misri

REUTERSAsmaa Waguih

Serikali ya Washington imewaonya raia wake kutoingia nchini Misri na kuwataka baadhi ya Wanadiplomasia wake kuondoka mara moja nchini humo kutokana na kuzorota kwa usalama. Onyo hilo limekuja kufuatia kuuawa kwa watu watatu katika ghasia hizo akiwamo raia mmoja wa Marekani mwenye umri wa miaka ishirini na moja.

Matangazo ya kibiashara

Mmarekani aliyeuawa akifanya kazi katika kituo cha utamaduni wa Marekani katika mji wa mwambao wa Aleksandria, na aliuawa wakati akichukua picha za maandamano hayo.

Hofu imeendelea kutanda kutokana na maandamano ya pande mbili kati ya wafuasi wanaomuunga mkono rais Mohamed Morsi na wapinzani wa serikali wanaowania kumng'oa madarakani ikiwa ni mwaka mmoja tu umepita tangu kuchaguliwa kwake.

Taarifa za mapema jumamosi hii zimearifu kuwa watu zaidi ya mia moja thelathini na watatu wamejeruhiwa katika machafuko hayo yanayozidi kushika kasi katika maeneo mbalimbali ya nchi.