DRCONGO-M23-UN

Wananchi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia wataka jeshi la Umoja wa Mataifa likabiliane na waasi

RFI

Jeshi la Umoja wa Mataifa lililoko nchini Jamhuri ya Kidekrasia ya Kongo limeelezwa kukufufua matumaini ya kurejea kwa amani mashariki mwa nchi hiyo.Wananchi wa DRC wamesema kuwa wanaliamini jeshi hilo kwa sababu lina nguvu na uwezo mkubwa lakini sasa hivi linalazimika kuingilia kati kwa kukabiliana na waasi wanasababisha uvunjifu wa amani.

Matangazo ya kibiashara

Wamesema kuwa jeshi hilo lazima likabiliane na waasi hao kwa sababu Serikali imekuwa ikifanya mazungumzo na waasi lakini hakuna makabaliano yenye mantiki yanayofikiwa.

Wananchi wa DRC wamebainisha hawayaamini mazungumzo ya Kampala Uganda ambayo yamekuwa yakisusua na kuongeza kuwa wakati umefika wa kuwawinda waasi na kukabiliana nao.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Machi 28 mwaka huu liliamua kupeleka kikosi cha wanajeshi 3,000 ambao tayari wameanza kujipanga kwa ajili ya kutekeleza jukumu lao.

Wanajeshi hao kutoka Malawi, Afrika Kusini na Tanzania wameungana na wanajeshi wengine 17,000 wa Umoja wa Mataifa ambao walikua tayari wanalinda amani wakiwa hawana mamlaka ya kupambana na waasi.

Jeshi la sasa la Umoja wa Mataifa limepewa mamlaka ya kujihami na kukabiliana na waasi wa M23 na wengine mashariki mwa nchi hiyo na kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo ubakaji.