SOMALIA

Mtu mmoja auawa kwa Shambulio la Bomu lililotekelezwa na Al Shabaab mjini Mogadishu

Moja ya Mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia
Moja ya Mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia REUTERS/Feisal Omar

Mtu mmoja ameuawa kwa Bomu na Wanamgambo wa Al Shabaab nchini Somalia baada ya kundi hilo kutega Bomu katika Soko moja mjini Mogadishu, lililokuwa na watu wengi waliokuwa kwenye pilikapilika za kibiashara wakati huu wakijiandaa na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Al Shabaab Abdulaziz Abu Musab amesema wapiganaji wake walitega mlipuko uliolenga Maafisa wa usalama katika Soko la Bakara mjini Mogadishu na kudai kuwa wamewaua maafisa watatu na kuwajeruhi wengine watatu.
 

Wanamgambo wa Al Shabaab wenye uhusiano na Kundi la kigaidi, Al Qaeda wameanza mashambulizi ya mfululizo ikiwemo Shambulizi la mwezi uliopita dhidi ya Ofisi za Umoja wa Mataifa.
 

Ingawa kundi hilo limekumbana na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe, pia kuuawa kwa Kiongozi wa kundi hilo, Wachambuzi wa mambo wanasema kundi hilo limeendelea kuwa hatari na gumu kulidhibiti.

Al shabaab imepoteza ngome zake katika miji waliyokuwa wakidhibiti, na kuchukuliwa majeshi ya Umoja wa Afrika ambayo yanapigana sambamba na Majeshi ya Serikali.
 

Hata hivyo, maeneo muhimu ya kundi hilo bado yameendelea kuwa katika maeneo ya kusini na katikati ya Somalia pia katika eneo la milima jimboni Puntland.