MALI

Watu wawili wajeruhiwa mjini Kidal baada ya mapigano yaliyosababishwa na hatua ya Vikosi vya Mali kuingia mjini Kidal

Wanamgambo wa MNLA nchini Mali
Wanamgambo wa MNLA nchini Mali AFP PHOTO / MNLA

Raia wawili wa Mali wako katika hali mbaya baada ya kupigwa risasi mjini Kidal, wakati huu ambapo kuekuwepo na mgogoro kwa kipindi cha siku tano baada ya Vikosi vya Kijeshi kuingia mjini Kidal kwa ajili ya kuweka mazingira ya utulivu kwa ajili ya Uchaguzi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano yalizuka mjini Kidal mji unaoshikiliwa na Waasi, baada ya Waasi wa Tuareg kuruhusu Jeshi la Mali kuingia mjini humo, ikiwa ni sehemu ya Makubaliano ya amani kwa ajili ya kupisha zoezi la kupiga kura la tarehe 28 mwezi huu.
 

Kidal, mji umekuwa ukidhibitiwa na Waasi wa MNLA tangu mwezi Januari lakini Waasi walikubaliana nchini Burkinafaso kuruhusu Vikosi vya kijeshi kuingia mjini humo.
 

Wanaounga mkono na wale wanaopinga Jeshi la Mali wamefanya maandamano na vurugu ambazo zilisababisha Walinda amani wa Umoja wa Mataifa na Mwanajeshi mmoja wa Ufaransa kujeruhiwa kwa mawe yaliyokuwa yakirushwa na wakati wa Maandamano mwishoni mwa Juma lililopita.
 

Udhibiti wa mji wa Kidal ulio mikononi mwa Waasi wa MNLA umekuwa kikwazo dhidi ya mchakato wa kuandaa uchaguzi, ambao ni muhimu kwa Taifa hilo baada ya kuwa kwenye Mgogoro kwa kipindi cha Miezi 18.
 

Gavana wa Mji wa Kidal alikuwa akitarajiwa kurudi mjini Kidal akitokea Bamako kwa ajili ya kuendelea na jukumu lake la uongozi katika maandalizi ya Uchaguzi lakini Safari yake iliahirishwa kutokana na sababu za usalama.
 

Wachambuzi wa Mambo wanashuku juu ya uwezo wa Mali kuandaa uchaguzi wa kuaminika , wakati huu ambapo takriban watu 500,000 wamekimbia nchi hiyo kutokana na Mapigano.