Sudani Kusini

Umoja wa Mataifa watoa wito kupelekwa kwa Vikosi vya kulinda amani nchini Sudani Kusini

Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir
Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC limetoa wito kwa Kikosi cha kulinda Amani Cha Umoja wa Mataifa UN kilichopo Sudan Kusini kupelekwa kwenye maeneo hatari ili kuwalinda wananchi ikiwa ni pamoja na kupatiwa zana za kisasa.

Matangazo ya kibiashara

Baraza la Usalama limetoa wito huo baada ya kupiga kura kuongeza muda wa Vikosi vya kulinda Amani kwa kipindi cha mwaka mmoja na kutaka wanajeshi zaidi kupelekwa katika Jimbo la Jonglei lenye machafuko ya kikabila.
 

Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa UN Francis Mading Deng amesema nchi yake ipo tayari kushirikiana na walinzi hao wa amani katika kuhakikisha wanadhibiti makundi ya wanamgambo na kuwalinda wananchi.
 

Marekani imesema kuwa iko tayari kusaidia Watu wa Sudani kusini walionasa kutokana na mapigano katika Jimbo la Jonglei ambapo Vikosi vya kijeshi vimekuwa vikipambana na Wanamgambo na kuwepo kwa Ukiukwaji wa Haki za Binaadam.
 

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jen Psaki amesema kuwa wanaguswa na Ripoti zinazoendelea kutolewa juu ya Ukiukwaji wa Haki za Binaadam ikiwemo mauaji, ubakaji, kupigwa, uporaji na uharibifu wa majengo na vifaa vya misaada katika Jimbo la Jonglei.
 

Psaki amezitaka pande zote likiwemo jeshi na wengine wote wanaojihusiaha na Mapigano, kukomesha machafuko hayo na kushirikiana katika kuleta amani na Maridhiano.
 

Jimbo la Jonglei ambalo ni kubwa zaidi nchini Sudani kusini limekuwa katika mapigano ya kikabila kwa kipindi cha zaidi ya Muongo mmoja, na madhara kwa Raia yamekuwa yakiongezeka.