MISRI

Familia ya Mohamed Morsi imepanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Al Sisi kwa kumshikilia mateka Kiongozi huyo

Wafuasi wa Kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohamed Morsi wakifanya maandamano huku wakiwa wamebeba picha zake
Wafuasi wa Kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohamed Morsi wakifanya maandamano huku wakiwa wamebeba picha zake REUTERS/Mohamed Abd El Ghany

Familia ya Rais aliyeondolewa madarakani nchini Misri Mohamed Morsi imetangaza itachukua hatua ya za kisheria dhidi ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Abdel Fattah Al Sisi kwa kuendelea kumshikilia mateka Kiongozi huyo wa Chama Cha Muslim Brotherhood.

Matangazo ya kibiashara

Mtoto wa Kike wa Morsi anayetambulika kwa jina la Shaimaa Mohamed Morsi ndiye ametangaza mpango huo wa kuchukua hatua za kisheria dhidi Jenerali Al Sisi aliyetangaza kwamba Kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani anashikiliwa na Jeshi.

Shaimaa ameweka wazi kabisa watachukua hatua hizo za kisheria kwa kuangalia sheria za ndani ya nchi hiyo na hata zile za kimataifa akimtaja mara kadhaa Jenerali Al Sisi kuwa aliongoza mapinduzi ya kumwaga damu ya kijeshi kumuondoa Baba yake madarakani.

Binti huyo wa Kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia na kukaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuondolewa amesema kile kinachofanywa na Jeshi ni utekejinyara na hivyo wao watachukua sheria dhidi ya hatua hiyo.

Shaimaa amewaambia wanahabari Jijini Cairo wamelitaka Jeshi kumuachia Morsi lakini lenyewe limeendelea kumshikilia kwa madai ya sababu za usalama na kiafya kitu ambacho kimeendelea kuwaacha bila majibu.

Familia ya Morsi imesema haijui sehemu ambayo Kiongozi huyo wa zamani anahifadhiwa kwa sababu jeshi halijawapa taarifa zozote na ndiyo maana wameona huu ni wakati muafaka wa kuchukua hatua za kishehia.

Mataifa ya Magharibi yakiwemo Marekani na Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya EU yalishatoa wito wa kuachiwa kwa Morsi lakini jeshi limeendelea kukaidi ombi hilo na badala yake lingali linamshikilia.

Shaimaa amesema baada ya kukataliwa kwa maombi hayo yote ndiyo maana wameona huu ni wakati muafaka wa kuchukua hatua za kisheria ili kuhakikisha Morsi anaachiwa baada ya kushikiliwa tangu kutangaza kwa mapinduzi yake na Jeshi.

Morsi anashikilia na Jeshi nchini Misri tangu kufanyika kwa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani tarehe 3 mwezi Julai ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Kiongozi wa Mpito Adly Mahmud Mansour.

Jeshi nchini Misri lilishatangaza hapo awali haliwezi kumuachia Morsi kwa sasa kwa sababu za kiusalama na kiafya kipindi hiki wafuasi wake wakiendelea kufanya maandamano ya nchi nzima kushinikiza kurudishwa kwake madarakani.