TOGO

Wananchi wa Togo wanapigakura kuchagua Wabunge wao huku Upinzani ukionya hawatokubali matokeo kukiwa na wizi wa kura

Mwanajeshi nchini Togo akipiga kura mapema siku ya Jumatatu kabla ya wananchi wengine kufanya hivyo Alhamisi
Mwanajeshi nchini Togo akipiga kura mapema siku ya Jumatatu kabla ya wananchi wengine kufanya hivyo Alhamisi

Wananchi wa Togo wanapigakura hii leo kuchagua wabunge nchini humo katika uchaguzi uliocheleweshwa hapo kabla kutokana na uwepo wa machafuko kipindi hiki wapinzani wakijiapiza kukiangusha Chama Tawala.

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika hapo kabla kutokana na Chama Tawala kushindwa kuitisha zoezi hilo kwa muda muafaka kitu ambacho kikachangia uwepo wa machafuko ya kushinikiza uchaguzi huo.

Upinzani nchini Togo umejiapiza kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kuumaliza utawala uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne uliokuwa unaongozwa na Familia ya Gnassingbe.

Serikali ya Togo imekuwa ikiongozwa na Familia ya Gnassingbe ambapo awali Gnassingbe Eyadema alianza kuongoza tangu mwaka 1967 hadi mwaka 2005 alipofikwa na umauti ndiyo mwanaye Faure Gnassingbe akachukua utawala.

Gnassingbe ameongoza Taifa hilo tangu mwaka 2005 na kuweza kushinda katika chaguzi mbili za mwaka huo na 2010 ambapo Upinzani ukajitokeza na kutamka kumekuwa na wizi wa kura na hila zilizomweka madarakani.

Uchaguzi huu wa Wabunge unafanyika kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo lifanye uchaguzi kama huo mwaka 2007 ambapo Chama Tawala kikashinda viti 50 kati ya 81 vilivyokuwa vinashindaniwa.

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Togo CENI imeamua kuongeza idadi ya viti na kufikia 91 kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya wawikilishi wa wananchi hivyo kutakuwa na kibarua kigumu cha kuwania viti hivyo.

Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Togo Jean Pierre Fabre ambaye pia anawania kiti cha ubunge ametoa onyo kali kwa serikali kuhakikisha hakuna wizi wowote wa kura na iwapo hilo litafanyika basi watajitokeza mitaani na kupinga.

Jeshi la Togo kwa muda wamekuwa wakipambana na wapinzani mitaani kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira tangu mwaka 2012 wakishinikiza kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge ulioshindikana kufanyika.