ZIMBABWE

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe aahidi uchaguzi huru na haki

Reuters/Philimon Bulawayo

Rais wa Zimbabwe Rober Mugabe amehitimisha kampeni zake za uchaguzi mkuu na kuwaahidi wananchi wake kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki. Akijinadi kwa mara ya mwisho amewasihi wapiga kura kumrejesha madarakani kwani atapambana na mataifa ya magharibi yanayotaka kuingilia uhuru wa Taifa lao.

Matangazo ya kibiashara

Raia nchini humo wanashiriki uchaguzi mkuu siku ya jumatano juma hili ikiwa ni miaka minne imepita tangu kuzuka kwa machafuko yaliyohitimishwa na uundwaji wa serikali ya muungano kati ya chama tawala ZANU-PF na chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC.

Uhusiano kati ya Mugabe na jumuiya ya kimataifa umeendelea kudorora kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, suala ambalo limepelekea nchi yake kuwekewa vikwazo.

Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai naye amewasihi wapiga kura kumchagua kwa kishindo ili arejeshe uhusiano kati ya Zimbabwe na jumuiya ya kimataifa kwani suala hilo litawezesha Taifa hilo kusonga mbele kiuchumi.

Wakati huo huo Polisi nchini humo inamshikilia Mshirika wa Waziri Mkuu Tsvangirai, baada ya kuripoti juu ya dosari za uchaguzi.

MDC Imesema Morgan Komichi alikamatwa baada ya kuileza tume ya uchaguzi kuwa Karatasi za kupiga kura zilizokuwa zimemchagua Morgan Tvangirai zilikutwa kwenye madebe ya kuweka takataka baada ya polisi wa usalama kupiga kura jijini Harare.

Komichi ambaye ni naibu Waziri wa Uchukuzi alikamatwa na askari nyumbani kwake, Msemaji wa Polisi amethibitisha kukamatwa kwake ikiwa ni siku tatu kabla ya uchaguzi mkuu.

Polisi imetishia kumshtaki Komichi kukiuka Sheria za uchaguzi ikiwa hataweka wazi juu ya nani alimpa taaarifa hizo.