Burundi-upinzani

Kiongozi wa chama cha waasi zamani nchini Burundi Agathon Rwasa aonekana hadharani baada ya kipindi cha miaka mitatu

Kiongozi wa chama cha FNL Agathon Rwasa
Kiongozi wa chama cha FNL Agathon Rwasa AFP PHOTO/ROBERTO SCHMIDT

 Kiongozi wa kihistoria wa kundi la uasi zamani nchini Burundi la FNL, Agathon Rwasa, ameonekana hadharani hii leo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu baada ya kukimbilia mafichoni ingawa polisi wamemzuia  kuhutubia umma wa wafuasi wake waliojitokeza kumkaribisha.

Matangazo ya kibiashara

Rwasa amewaambia waandishi wa habari huko villa kwenye mji mkuu wa Bujumbura , kuwa miaka mitatu iliyopita, alilazimika kuwaacha watu wake wa karibu ili kunusuru maisha yake ,kutokana na mzozo uliotokana na uchaguzi, na kuongeza kuwa hii leo anamaliza muda wake wa kukaa mafichoni kuitika wito wa kurejea nyumbani na kuongoza chama chake.

Akiwa amevalia nadhifu suti ya rangi ya bluu na tai nyekundu, kwa mara ya kwanza Rwassa amejitokeza katika ukumbi wa ndani wa jamii ambapo wafuasi wake walikuwa wakiadhimisha kurudi kwake

Maafisa kadhaa wa Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia wa kigeni pia walikusanyika kushuhudia kurudi kwake lakini maafisa kadhaa wa polisi walimzuia Rwasa na kumrudisha nyuma, wakisema kwamba hakuwa na mamlaka muhimu ya kufanya mkutano.

Awali msemaji  wa Rwasa aliarifu kuwa kiongozi huyo anakuja kukusanya wafuasi wake na kuwaweka pamoja kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 ambapo atawania kiti cha urais.

Juni 2010 Agathon Rwasa alirejea mafichoni kwa kile alichodai anahofia usalama wake. Hata hivyo mauaji ya hapa na pale yalifuatia kutoroka kwa kiongozi huyo aliye vikwa lawama na kundi lake kuhusika katika mauaji hayo.

Serikali ya Burundi ilimchukulia kiongozi huyo kama kiongozi hatari sana kwa usalama wa taifa hilo na kuanzisha harakati za kumsaka bila mafaanikio.

Aime Magera amesema kwamba kiongozi huyo wa upinzani aliachana na uasi na hawezi tena kureja msituni, na kwamba hajawahi kuhamasisha vurugu kama inavyo daiwa. Ameongeza kwamba jamii ya kimataifa imechangia pakubwa katika hatuwa hii.

Duru za kidiplomasia zimethibitisha taarifa hii na kuongeza kuwa juhudi za jamii ya  kimataifa zimefaanikisha kumrejesha kiongozi huyo baada ya kukubali kuwa hatoendelea kuukana utawala uliopo.

Tangu mwaka 2010, Agathon Rwasa alitajwa kukimbilia nchini DRCongo katika mkoa wa kivu ya kusini, Tanzania na Zambia, lakini msemaji wake amesema kiongozi huyo hajawahi kutoka katika ardhi ya Burundi, na alikuwa akijificha miongoni mwa wananchi ambao walimuhudumia kwa kipindi chote hiki.