Mali

Raia wa Mali wasubiri matokeo ya duru la pili la uchaguzi

Mgombea wa Urais nchini Mali, Soumaila Cissé akipiga kura
Mgombea wa Urais nchini Mali, Soumaila Cissé akipiga kura AFP PHOTO / HABIBOU KOUYATE

Wananchi nchini Mali wanasubiri matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais baada ya kupiga kura siku ya Jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Kinyanganyiro kikali ni kati ya Waziri Mkuu wa zamani Ibrahim Boubacar Keita na aliyekuwa Waziri wa fedha Soumaila Cisse .

Uchaguzi wa Mali unatarajiwa kuleta hali ya utulivu na uthabiti wa kisiasa nchini humo baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka uliopita.

Takriban wapigakura milioni saba walipiga kura mwishoni mwa juma lililopita, uchaguzi wa kwanza tangu mwaka 2007 ambao pia ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa uchumi wa Taifa la Mali

Waangalizi wa uchaguzi huo kutoka umoja wa ulaya wanatarajiwa kutoa Ripoti yenye kutathimini mwenendo wa uchaguzi hii leo.Waangalizi w Uchaguzi huo wanasema zoezi hilo lilikwenda vizuri.

Waangalizi huru wa uchaguzi takriban 2,000 walitoa tamko kuwa uchaguzi ulikuwa wenye utulivu lakini walieleza dosari za kuchelewa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura mjini Bamako na kusini mwa mji wa Koulikoro na Kayes.
 

Kwa upande wa Wagombea wa Urais Keita na Cisse kwa pamoja wamekuwa wakijiamini kushinda uchaguzi huo.
 

Kurejea kwa utawala wa kidemokrasia nchini Mali kutairuhusu ufaransa kuondoa vikosi vyao 4,500 walioingia nchini Mali mwezi Januari kwa ajili ya kupambana na wanamgambo wa kiislamu waliokuwa wamedhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, baada ya mapinduzi ya kijeshi.