DR Congo

Mashirika ya kiraia nchini Congo kugoma kushinikiza vikosi vya UN kuanza kazi ya kunyang'anya silaha waasi

Waasi wa M23 ambao ni moja ya makundi yanayohatarisha usalama wa Raia Mashariki mwa Congo
Waasi wa M23 ambao ni moja ya makundi yanayohatarisha usalama wa Raia Mashariki mwa Congo

Muungano wa mashirika ya kiraia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC umetangaza kuitisha mgomo na maandamano kwenye maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kushinikiza kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa UN kilichoko nchini humo kuanza kazi ya kuwanyang'anya silaha Waasi.

Matangazo ya kibiashara

Wito huo wa mashirika ya kiraia unakuja wakati huu ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ubelgiji Didier Rynders akifanya ziara nchini humo kuzungumzia hali ya usalama mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza na idhaa ya kiswahili rfi wakati wa mahojiano na mwandishi wetu Ruben Lukumbuka, Naibu mwenyekiti na msemaji wa muungano wa mashirika hayp, Omar Kavota anasema hatua hiyo haitaathiri kwa vyovyote jitihada za jumuiya ya kimataifa bali wanachotaka wao ni kuona hatua zinachukuliwa sasa.

Katika hatua nyingine Mashirika ya kutetea haki za watoto na wanawake nchini DRC yanaitaka serikali ya nchi hiyo kuunda mahakama maalumu itakayotumika kusikiliza kesi dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya ubakaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.

Mkuu wa shirika la kutetea maslahi ya watoto na wanawake nchin DRC, Gogo Kavira amesema kuwa wakati umefika kwa Serikali ya DRC kutengeneza mahakama maalumu ambayo itakuwa na jukumu la kusikiliza kesi dhidi ya uhalifu wa kibinaadamu unaofanyika mashariki mwa nchi hiyo.

Mkuu huyo ameongeza kuwa kuundwa kwa mahakama hii ndio njia pekee ya kuhakikisha haki inatendeka kwa wale wote walioathirika na vitendo hivi lakini kwa watuhumiwa wa makosa ya ubakaji na nyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, vitendo ambavyo vinaendelea kukithiri wakati huu mapigano yakiendelea.