Mali

Ibrahim Boubakar Keita awa mshindi wa Duru la pili la uchaguzi nchini Mali

Mshindi wa duru la pili la uchaguzi nchini Mali Ibrahim Boubacar Keïta
Mshindi wa duru la pili la uchaguzi nchini Mali Ibrahim Boubacar Keïta REUTERS/Joe Penney

Waziri Mkuu wa zamani Ibrahim Boubacar Keita ndiye ambaye ameibuka mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Mali, mpinzani wake Soumaïla Cisse aliyeshiriki naye katika kinyang'anyiro hicho amempongeza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya raundi ya pili ya uchaguzi uliyofanyika siku ya jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Vyanzo vya habari vya Tume ya uchaguzi na usalama awali vilisema kuwa Keita alikuwa akiongoza kwa asilimia kadhaa kwa kura zilizohesabiwa baada ya uchaguzi wa duru la pili, za mwishoni mwa juma lililopita.

Uchaguzi huu umemalizika na sasa umefungua milango ya kuanza upya kwa Taifa la Mali ambalo kwa zaidi ya mwaka mmoja limekuwa katika mgogoro wa Kisiasa tangu baada ya Mapinduzi ya kijeshi

uchaguzi huu ambao ni wa kwanza tangu mwaka 2007, umeonekana kuwa muhimu kwa ajili ya mustakabali wa kiuchumi wa Mali, hasa katika kurejesha msaada wa Yuro Bilioni 3 zilizoahidiwa na Wahisani wa kimataifa ambao walisitisha mchango wao baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha kuzuka kwa makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali.

Changamoto kadhaa zilikumba uchaguzi wa Mali hasa mjini Bamako, na Waangalizi wa Umoja wa Ulaya wametoa tathimini kuwa takriban asilimia 45 ya watu walipiga kura idadi ndogo kuliko ya durua la kwanza ambapo asilimia 48.9 ya wapiga kura walijitokeza hata hivyo idadi hii imeelezwa kuwa kubwa kuliko chaguzi za miaka ya nyuma.

Mkuu wa Sera za Mambo ya nje ndani ya Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton amepokea kwa mikono miwili uchaguzi huu aliouita wa huru na wa kuaminika na kutaka pande zote zilizoshiriki uchaguzi kuunga mkono matokeo na kusaidia kujenga mustakabali wa mali, kujenga amani ya kudumu na Umoja wa kitaifa.
 

Kurejea kwa utawala wa kidemokrasia nchini Mali kunaipa fursa ufaransa kuondoa vikosi vyake 4,500 waliopelekwa nchini Mali mwezi Januari kwa lengo la kusambaratisha makundi ya Wanamgambo wenye uhusiano na Al Qaeda waliokuwa wakidhibiti eneo la kaskazini mwa Mali.