DR Congo

Kanali wa Jeshi la Serikali ya Congo aasi Jeshi pamoja na Wanajeshi wengine takriban 60

Waasi wa M23 ambao ni moja ya makundi yanayohatarisha usalama wa Raia Mashariki mwa Congo
Waasi wa M23 ambao ni moja ya makundi yanayohatarisha usalama wa Raia Mashariki mwa Congo REUTERS/Goran Tomasevic

Kanali ndani ya Jeshi la Serikali ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo pamoja na Watu wake wengine ndani ya jeshi hilo takriban 60 wameasi Jeshi na kujiunga na Waasi wa M23 ambao wamekuwa wakizorotesha hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kanali Richard Bisamaza ametoroka na Watu wake takriban 60 mapema jana asubuhi, Luteni Kanali wa Jeshi la Serikali, Kanali Olivier Hamuli ameliambia shirika la Habari la Ufaransa, na kuongeza kuwa uamuzi huo si wa kushtusha,ikizingatiwa asili ya Bisamaza.
 

Hamuli amesema kuwa kuondoka kwa Kanali huyo hakutaathiri jeshi hilo, na kuwa Wanapenda kuwa na Jeshi lisilo na Watu ndumila kuwili.
 

Bisamaza mwenye asili ya Jamii ya Tutsi, alipaswa kusafiri kutoka katika kambi iliyopo jimbo la Kivu kaskazini kuelekea Kinshasa kwa ajili ya shughuli maalum lakini badala yake alitokomea msituni kujiunga na Waasi wa M23.
 

Hamuli amemshutumu Bisamaza kujiunga na M23 walio na maskani yao karibu na eneo la mpaka wa Congo na Rwanda, ambapo kwa mujibu wa Hamuli kundi hilo linafadhiliwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Uganda.
 

Nchi ya Uganda na Rwanda zimekua zikishutumiwa na Umoja wa Mataifa kuunga mkono uasi huku nchi hizo zikikana shutuma hizo.
 

Kutoroka kwa Wanajeshi hao kumefanyika ikiwa ni siku ya kwanza tangu kuanza kazi kwa Mwanadiplomasia wa Ujerumani Martin Kobler ambaye anaongoza Operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imepewa jukumu la kutumia nguvu kunyang'anya silaha makundi ya Wapiganaji.