Mali

Rais Mteule wa Mali Ibrahim Boubacar Keita aanza jukumu la kuwaunganisha Raia wa Mali

Rais Mteule wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta.
Rais Mteule wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta. Pierre René-Worms / RFI

Rais mteule wa nchini Mali, Ibrahim Boubacar Keita ameanza jukumu la kupanga mkakati kuiponya Mali kutokana na Mzozo wa kisiasa, Mapinduzi ya kijeshi na Mapigano.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo Rasmi nchi nzima bado hayajatangazwa lakini mpinzani wa Keita, Somaila Cisse amempongeza Keita kwa ushindi baada ya kumshinda kwenye duru la pili la uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa juma lililopita.
 

Uchaguzi wa kwanza wa Mali tangu Mwaka 2007 umeonekana kuwa muhimu sana kwa mustakabali wa uchumi wa nchi hiyo hasa baada ya Mataifa Wahisani kusitisha msaada wa fungu la fedha baada ya mapinduzi ya kijeshi ambayo yalisababisha kuzuka kwa uasi hali iliyofanya majeshi ya Ufaransa kuingilia kati.
 

Serikali ina siku mpaka ya ijumaa kutangaza hadharani matokeo ya Duru la pili la uchaguzi.
 

Wakati wa Kampeni, Keita aliahidi kuwaunganisha Watu wa Mali baada ya kuwa katika msukosuko na kile alichokiita kujidhalilisha kwa kuomba msaada wa Ufaransa kupambana na Waasi waliokuwa wanadhibiti eneo la kaskazini mwa Mali.
 

Keita ameahidi kuleta amani na usalama na kuanzisha mazungumzo ya kitaifan na kujenga Taifa lenye msingi wa heshima, utu, kujiamini na lenye kuwajibika kwa bidii.
 

Ingawa Cisse alilalamika kuwa zoezi la kura lilijawa na udanganyifu, aliwaambia Waandishi wa habari kuwa hatapeleka shauri mahakamani kupinga matokeo akizingatia hali ya sasa ilivyo nchini humo.
Waangalizi wa uchaguzi huo toka Umoja wa ulaya wametoa tathimini Chanya juu ya uchaguzi huo.
 

Jumuia ya kimataifa imepokea kwa mikono miwili matokeo ya uchaguzi huo huku Chanzo cha habari kutoka Ofisi ya Rais wa Ufaransa, Francois Hollande kimesema kuwa Rais huyo ataelekea Mali kuhudhuria Sherehe za kuapishwa kwa Keita.
 

Marekani nayo imesemakuwa inajiandaa kufungulia tena misaada kwa nchi ya Mali baada ya uchaguzi, huku Waziri wa Uingereza kwa Maswala yahusuyo Afrika, Mark Simmonds, ametoa wito kwa Keita kuweka Tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Wabunge.