JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa latoa wito wa kurejesha hali ya utulivu nchini Afrika ya kati

Wanamgambo wa Seleka wakiwa katika Operesheni yao jijini Bangui
Wanamgambo wa Seleka wakiwa katika Operesheni yao jijini Bangui REUTERS/Alain Amontchi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa hali ya mfarakano nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati imekuwa tishio nchini humo na katika eneo la Afrika ya Kati, na kutoa wito wa kuchukua hatua za kurudisha hali ya utulivu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Tamko hilo lilitolewa na nchi wanachama 15 wa Baraza la usalama la umoja wa Mataifa halijatanabaisha namna mpya ya kukabiliana na mzozo, lakini Ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon imetoa wito wa kuwekwa vikwazo dhidi ya maafisa kutoka kwa Umoja wa Seleka wanaoshutumiwa kujihusisha na ukiukwaji wa haki za binaadam.
 

Kwa mujibu mwa Mwakilishi wa UN Babacar Gaye, vitisho vya Vikwazo vinalenga kushinikiza nchi hiyo kuboresha na kuheshimu haki za binaadam nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati.
 

Nchi hiyo iliingia katika machafuko baada ya Waasi wa Seleka kudhibiti maeneo ya nchini humo na kufanya vitendo vya mauaji na uporaji.
 

Baraza la usalama limesema kuwa usalama umedorora nchini humo na kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa Sheria, pia ukosefu wa utawala wa Sheria.
 

Vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadam vinavyodaiwa kutekelezwa na Waasi wa Seleka ni pamoja na Kuwakamata watu hovyo, kuwashikilia na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto,utesaji, ubakaji na mauaji, pia wamekuwa wakiwasajili watoto katika kundi lao na kuwatumia kutekeleza mashambulizi dhidi ya Raia.
 

Shirikisho la Kimataifa la kutetea haki za binaadam lilisema mwezi uliopita kuwa umeweka Rekodi ya Matukio takriban 400 ya Mauaji yaliyofanywa na Kundi la Seleka tangu Mwezi March.
 

Kwa mujibu wa Takwimu za Umoja wa Mataifa, Watu milioni 1.6 nchini Jamuhuri ya Afrika ya kati wanahitaji msaada wa haraka. Mzozo wa nchini humo umesababisha Watu 60,000 kukimbilia nchi za jirani. Mpaka sasa Watu 206,000 wameyahama makazi yao.