Egypt

Zaidi ya Watu 500 wauawa kwenye Machafuko nchini Misri

Miili ya Watu waliouawa wakati wa machafuko ya nchini Misri
Miili ya Watu waliouawa wakati wa machafuko ya nchini Misri REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Raia wa Misri wameendelea tena hii leo na shughuli zao baada ya kuwepo kwa hali ya hatari usiku mzima baada ya Watu zaidi ya 500 kuuawa wakati Vikosi vya usalama vilipokuwa vikiwatawanya Waandamanaji wanaomuunga mkono aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Morsi.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi linalounga mkono Serikali ya mpito lilitangaza hali ya taadhari nchi nzima kwa kipindi cha mwezi mmoja na hali ya hatari jijini Cairo na majimbo mengine 13.
 

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa muda wa hali ya hatari hii leo asubuhi, taa za kuongoza magari barabarani ziliwaka tena katika mitaa ya jiji la Cairo, na barabara zilizokuwa zimefungwa kwa majuma kadhaa na Wafuasi wa Morsi zilifunguliwa.
 

Wizara ya Afya ilitangaza kuwa Takriban Raia 300 wameuawa na kuongeza kuwa Wana kikosi wa usala 43 wameuawa.
 

Ghasia hizi ni mbaya zaidi kutokea, tangu zile za mwaka 2011 ambazo zilimuondoa aliyekuwa Rais wa Taifa hilo Hosni Mubarak, ambapo Chama cha Muslim Brotherhood kimesema kiwa Watu 2,200 wameuawa na zaidi ya 10,000 wamejeruhiwa.
 

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais wa Misri,Mohamed El Baradei amejiuzulu akisema kuwa anafadhaishwa na namna ambavyo Watu wamekuwa wakipoteza maisha wakati matukio hayo yangeweza kuepukika.
 

Operesheni hizo zilizanza kwa Vikosi vya usalama vilipotumia Gesi ya kutoa machozi dhidi ya Waandamanaji waliokuwa wamekita Kambi kukemea mapinduzi dhidi ya Morsi.