Misri

Chama cha Muslim Brotherhood chapanga Maandamano mapya nchini Misri hii leo

Waandamanaji wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiwa mtaani jijini Cairo
Waandamanaji wanaomuunga mkono Mohamed Morsi wakiwa mtaani jijini Cairo REUTERS/Stringer

Wafuasi wa Chama cha kiislamu cha Muslim Brotherhood waitisha maandamano siku ya leo kudhihirisha ghadhabu zao baada ya kuuawa kwa Watu takriban 600 wakati vikosi vya usalama vilipokuwa vikisambaratisha makambi yaliyowekwa na Wafuasi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mohamed Morsi.

Matangazo ya kibiashara

Wito huu umeongeza hofu ya kuzuka kwa machafuko baada ya yale ya siku ya jumatano hali iliyosababisha Umoja wa Mataifa kukemea Machafuko hayo na kutaka kusitishwa mara moja na pande zote mbili.
 

Hali ya hatari imetangazwa katika majimbo mengi ya nchini Misri huku kukiripotiwa kuuawa kwa Wanajeshi saba na Askari mmoja kuuawa katika mji wa Assiut.
 

Wizara ya mambo ya ndani imetoa amri kwa Askari kutumia risasi iwapo majengo ya Serikali yatashambuliwa.
 

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa limekemea yanayojiri nchini Misri na kuitisha mkutano wa dharura juu ya Misri, hatua iliyoombwa na Ufaransa, Uingereza na Australia.
 

Msemaji wa makundi ya kiislamu yanayomuunga mkono Morsi, Laila Moussa amesema kuwa yamepangwa maandamano nchi nzima hii leo na kuongeza kuwa wafuasi wa Morsi wakiwemo Wabunge wa zamani wamekamatwa wakati wa maandamano .
 

Jijini NewYork Balozi wa Agentina ndani ya Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Maria Cristina Perceval, amesema kuwa Wanachama wa Baraza la usalama la umoja wa Mataifa wanasikitishwa na namna ambavyo Wamisri wamekuwa wakipoteza maisha jijini Cairo na kutoa wito wa kufanyika maridhiano ya kitaifa.
 

Jijini Washington, Rais wa Marekani, Barack Obama amesitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Misri kutokana na yanayojiri hivi sasa nchini Misri.
 

Halikadhalika Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa wito kwa Raia wake kutosafiri kwenda Misri na kuwataka Wamarekani walio nchini Misri, kuondoka.