Mali

Mali yamtangaza rasmi Ibrahim Boubacar Keita kuwa mshindi wa duru la pili la uchaguzi

Rais Mteule wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta.
Rais Mteule wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta. REUTERS/Joe Penney

Mali imemtangaza Ibrahim Boubacar Keita kuwa Kiongozi mpya siku ya Alhamisi baada ya kuthibitishwa kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Taifa hilo kuwa ameshinda duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika jumapili juma lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa juu ya matokeo hayo, Keita ameongoza kwa asilimia 77.6 ya kura zilizopigwa huku mpinzani wake akipata asilimia 22.4 ya Kura.

Waliojitokeza kupiga kura ni asilimia 45.8, Waziri wa mambo ya ndani Moussa Coulibaly ameeleza, na kuongeza kuwa kura 93,000 ziliharibika ikilinganishwa na kura 400,000 zilizoharibika katika duru la kwanza la uchaguzi.
 

Uchaguzi wa Mali ni wa kwanza tangu mwaka 2007 na umeonekana muhimu zaidi kwa mustakabali wa uchumi wa Mali, kwa kuhakikisha kuwa mataifa ya magharibi yaliyositisha misaada nchini Mali kwa sababu ya mapinduzi ya kijeshi wanarejesha tena misaada hiyo nchini Mali.
 

Cisse Aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Mali alikubali kushindwa na Keita katika Duru la Pili la uchaguzi kabla ya Keita kutangazwa rasmi kuwa Mshindi.
 

Utawala wa Keita umeanza huku kukiwa na ukosoaji mkubwa baada ya Kiongozi wa Mapinduzi ya kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo kupandishwa Cheo pamoja na kuwa aliongoza mapinduzi dhidi ya Serikali ya Mali chini ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Amadou Toumani Toure.
 

Wizara ya ulinzi imesema kuwa Baraza la Mawaziri limeridhia kuteuliwa kwa Kapteni Sanogo kuwa Luteni Jenerali wa Jeshi la Mali siku mbili baada ya Ibrahim Boubacar Keita kuibuka Rais Mteule.
 

Shirika la kimataifa la Waangalizi wa haki za binaadam Humman Rights Watch limesema kuwa kitando cha kumpa cheo Sanogo ni cha aibu.
 

Mtafiti ndani ya Shirika hilo Corinne Dufka,amesema Badala yake Kepteni Sanogo angepaswa kufanyiwa uchunguzi juu ya shutma za kujihusisha na vitendo vya kutesa na kujihusisha na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binaadam.