AFRIKA KUSINI

Wafanyakazi 34 wa Mgodi wa Marikana waliouawa nchini Afrika kusini wakumbukwa hii leo

Maandamano ya Wafanyakazi wa mgodi wa Marikana walipokuwa wakifanya Maandamano, mwaka 2012
Maandamano ya Wafanyakazi wa mgodi wa Marikana walipokuwa wakifanya Maandamano, mwaka 2012 REUTERS/Mike Hutchings

Maelfu ya Wafanyakazi wa Mgodi na wanafamilia wa Wafanyakazi wa mgodi 34 waliouawa na Polisi wa nchini Afrika kusini wakati wa ghasia zilizotokea baada ya mgomo wa Wafanyakazi wa Mgodi wamefanya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea kwa vifo hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Watu mbalimbali walikusanyika katika eneo la mgodi wa Marikana ambalo Tarehe 16 mwezi Agosti mwaka 2012 palitokea Ghasia zilizoushtua ulimwengu.

Viongozi wa dini walifanya ibada ya pamoja kuwaombea waliopoteza maisha kwenye Ghasia hizo, Watu watanyamaza kimya katika muda uleule ambao tukio la mauaji lilitokea na kuwataja waliopoteza maisha kwa majina.

Katika tukio hilo la mauaji Takriban Watu wengine 10 waliuawa wakiwemo askari wakati wa ghasia hizo zilizosababishwa na Wafanyakazi wa Mgodi kudai mazingira mazuri ya kufanya kazi pia nyongeza ya mshahara.

Kumbukumbu hiyo inafanyika wakati huu ambapo hakuna anayeshikiliwa kuhusika na vifo vya Wafanyakazi hao.

Wakati huu wa kumbukumbu ya kuuawa kwa Wafanyakazi wa Mgodi, Kamishna wa Polisi ametoa wito kwa Raia kuwa katika hali ya utulivu na kuwaonya kutobeba silaha hatari.
Chama tawala, ANC kilisema hakitashiriki kwenye shughuli za kumbukumbu hizi kwa kuwa haitambui waandaaji hasa kwa kuhofu kuwa shughuli hiyo huenda ikageuzwa katika misingi ya kisiasa.
 

Siku mbili kabla ya kumbukumbu Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma alitoa tamko la kuwepo kwa amani, maombi na tafakari kwa siku ya leo.
 

Shughuli ya hii leo imeandaliwa na kundi lililo chini ya Mwamvuli wa Jumuia ya Wafanyakazi wa Mgodini.