SOMALIA

Serikali ya Somalia yatimiza mwaka mmoja wakati hali ya usalama ikiwa bado ni tete

Rais wa Somalia wakati wa kuchaguliwa kwake
Rais wa Somalia wakati wa kuchaguliwa kwake

Leo ni mwaka mmoja toka Serikali mpya ya Somalia iingie madarakani na pia kumalizika kwa uasi wa wanamgambo wa Al-Shabab nchini humo waliofurushwa na vikosi vya Umoja wa Afrika AU na vile vya majeshi yaa Kenya KDF.

Matangazo ya kibiashara

Lakini wakati mwaka mmoja ukitimia matumaini ya wananchi wa Somalia kuona taifa lao likirejea kwenye hali ya utulivu na amani yamekumbwa na sintofahamu kufuatia mashambulizi ya kujitoa muhanga yanayoendelea kushuhudiwa na kutoa shangwe kidogo tu kwa serikali mpya ya Somalia ambayo inatimiza mwaka mmoja.

Pigo kubwa kwa nchi ya Somalia ndani ya mwezi huu ni pale madaktari wasio na mipaka MSF kutangaza kufunga ofisi zao nchini Somalia kwa kile shirika hilo linachodai kukosekana kwa usalama wa kutosha nchini humo na pia kwa wafanyakazi wake.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuwa Serikali ya Somalia inayoongozwa na rais Hassan Sheikh Mohamud imeshindwa kutoa hakikisho la usalama kwa wananchi wake na hata kuweka utawala imara kwenye mji mkuu Mogadishu.

Zaidi ya raia wa Somalia wapatao milioni ni wakimbizi na wanaishi nje ya nchi yao huku wengine milioni ni wakimbizi na hawana makazi ndani ya Somalia huku umoja wa mataifa UN ukionya kuhusu kukithiri kwa vitendo vya ubakaji.