KENYA-SOMALIA

Maelfu ya wakimbizi katika kambi ya Dadaab nchini Kenya wanapiga kura

Wakimbizi katika kambi ya Dadaab Kaskazini Mashariki mwa Kenya wanapiga kura kuwachagua viongozi wao.

Matangazo ya kibiashara

Huu ni uchaguzi muhimu sana kwa maelfu ya wakimbizi hao kutoka nchini Somalia ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi nchini Kenya kutokana na ukosefu wa usalama na kuwepo kwa njaa katika taifa lao.

Miongoni mwa nyadhifa zinazowaniwa katika uchaguzi huo ni pamoja na kiongozi wa kambi hiyo kubwa zaidi duniani, wawakilishi wa akina mama na vijana.

Kampeni zilimalizika mwishoni mwa Juma lililopita na tayari uchaguzi huo unafanyika chini ya uangalizi wa mashirika yanayotetea maslahi ya wakimbizi .

Wakimbizi waliosajiliwa ndio wanaoruhusiwa kupiga kura na viongozi watakaochaguliwa watawaakilisha katika mikutano ya wakimbizi na pia kuwasilisha matatizo yao kwa wahisani.

Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilitangaza kuwa tayari wakimbizi 80,000 kutoka nchini Somalia wamerudi nyumbani kwa hiari huku juhudi zikifanyika kuwashawishi wakimbizi zaidi kufanya hivyo.

Kenya inasema tayari imeisaidia Somalia kupata amani na wakati umefika kwa wakimbizi hao zaidi ya Laki tano kurudi nyumbani ili kulijenga taifa lao, lakini serikali ya Somalia na shirika la wakimbzi duniani UNHCR linaomba muda zaidi kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.

Kongamano la kimataifa linatarajiwa kufanyika jijini Nairobi kati ya tarehe 28 na 29 mwezi wa huu wa Nane chini ya rais Uhuru Kenyatta na kuhudhuriwa na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamed,na viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi kujadili suala hili.

Mwaka 2011 jeshi la Kenya liliingia nchini Somalia kupambana na wanamgambo wa Al-Shabab na kufanikiwa kuwaondoa katika ngome yao ya Kismayo.