DRC

Serikali DRC yawaelimisha raia kuhusu jeshi la MONUSCO

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo  imewatuma Mawaziri sita mjini Goma Mashariki mwa nchi hiyo  kutoa elimu kwa raia kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MONUSCO ambalo raia wanasema limeshindwa kuwalinda dhidi ya waasi.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na kukutana na raia, Mawaziri hao pia wamekuwa wakishauriana na viongozi wa MONUSCO kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono katika juhudi zao za kulinda amani Mashariki mwa nchi hiyo.

Ziara hii inakuja wakati MONUSCO ikifanya uchunguzi kuhusu tuhma kuwa wanajeshi wake waliwapiga risasi na kuwaua waandamanaji wawili mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Goma.

Nao Umoja wa Ulaya umeshtumu kuzuka upya kwa mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali Mashariki mwa nchi hiyo  na kutaka waasi kuweka silaha chini.

EU inasema makabiliano yaliyozuka kati ya waasi wa M 23 na majeshi ya serikali wiki iliyopita yanadidimiza matumaini ya kupatikana kwa amani ya kudumu katika eneo hilo.

Ukosefu wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeilazimu serikali ya Uingereza kuwaagiza  raia wake wote wanaoishi na kufanya kazi mjini Goma kuondoka kwa kuhofia usalama wao.

Kiongozi wa kundi la M 23 Betrand Bissimwa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akilalamikia kuhusika kwa jeshi la kulinda amani katika mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo na kutekeleza mauaji .

Jeshi la serikali kwa upande wake linasema kuwa litaendelea kulinda mipaka ya nchi hiyo na pia kukabiliana na makundi ya waasi likiwemo la M 23 ikiwa litaanza kuwavamia.

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kinsasha na waasi wa M 23 yamegonga mwamba jijini Kampala Uganda suala ambalo limeendelea kuhatarisha usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa ukiendelea kwa kipindi kirefu na ulizorota mwaka uliopita baada ya kuzuka kwa kundi la M23 lililodai kubaguliwa na serikali ya Kinsasha.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikituhumiwa na jirani zao DRC na Umoja wa Mataifa kufadhili na kuwaunga mkono waasi wa M 23 tuhma ambazo Kigali imeendelea kukanusha.

Jeshi la kulinda la umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini tayari liko Mashariki mwa nchi hiyo kukabiliana na makundi ya waasi.