SUDAN

Waasi katika jimbo la Darfur nchini Sudan wakutana kujadili amani

Mpatanishi wa mgogoro wa jimbo la Darfur nchini Sudan Mohamed Ibn Chambas, amesema kuwa atawasilisha ripoti kwa serikali ya Khartoum kuhusu mazungumzo ya amani ambayo amekuwa akiyaongoza kati ya makundi pinzani ya waasi katika jimbo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Chambas amesema kuwa mazungumzo hayo yamekuwa yakifanyika mjini Arusha nchini Tanzania kati ya waasi wa Justice and Equality Movement (JEM) na wale wa Sudan Liberation Movement kundi  linaloongozwa na Minni Minnawi (SLM-MM) na juhudi zimepigwa kupata suluhu la kudumu .

Waasi hao wamekuwa wakishawishiwa na mpatanishi huyo kukubali kuketi katika meza moja ya mazungumzo chini ya mkataba wa amani wa Doha ili kuanza kwa mazungumzo kuhusu mzozo huo.

Mazungumzo kati ya makundi haya mawili yamefanyika miaka miwili baada ya kutiwa kwa mkataba huo wa amani kati ya makundi hayo ambayo kwa zaidi ya miaka kumi yameendelea kupigana na serikali ya Sudan.

Juhudi za mazungumzo zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na makundi hayo ya waasi kugawanyika kuhusu namna ya kutatua mzozo huo kati yao na serikali ya Sudan pamoja na mgogoro wa uongozi kati yao.

Chambas anawataka viongozi wa makundi hayo kuketi katika meza ya mazungumzo na kupata suluhu ya kudumu ili kumaliza ukosefu wa usalama katika jimbo hilo na kumalizika kuteseka kwa raia wasiokuwa na hatia.

Mpatanishi huyo ameongeza kuwa waasi wamekubali kukutana baada ya miezi miwili kujaribu kupanga mikakati ya kupata suluhu ya kudumu kwa mzozo wa amani katika jimbo hilo.

Machafuko katika jimbo la Darfur yalianza mwaka 2003 baada ya waasi wa JEM na wale wa SLM/A kuchukua silaha na kuanza kukabiliana na majeshi ya serikali ya Sudan kwa madai kuwa serikali ya rais Omar Al Bashir ilikuwa inawabagua kwa sababu wao hawana asili ya kiarabu.

Serikali ya Sudan iliwahami waasi wa Janjaweed ambao walianza kuwasaka watu weusi katika jimbo hilo na kuwaua katika machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Rais Bashir Al Bashir anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa makosa ya mauaji ya maelfu ya watu na makosa mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu.