LIBERIA

Wanafunzi zaidi ya 25,000 waanguka mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu Liberia

Wizara ya elimu nchini Liberia imetangaza kuwa zaidi ya wanafunzi 25,000 walishindwa kupita mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Liberia. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa elimu Etmonia David-Tarpeh amesema kuwa ameshangazwa na kuanguka kwa wanafunzi hao wengi ambao hawakuweza hata kujieleza kwa lugha ya Kiingereza.

Hii inakuja siku chache baada ya rais Ellen Johnson Sirleaf ambaye amewahi kushinda taji la amani la Nobel kusema kuwa serikali yake inakabiliwa na hali ngumu ya kuhakikisha kuwa raia wake wanapata elimu bora.

Liberia ambayo ilikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu kwa kiasi fulani iliathiri sekta ya elimu ambapo watoto badala ya kwenda shule walipewa silaha kwenda kupigana.

Shule nyingi nchini Liberia hazina walimu wa kutosha, vitabu vya kusoma na pia ukosefu wa madarasa mazuri yamechangia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi kushindwa kufanya vizuri.

Hii ndio mara ya kwanza kwa wanafunzi waliotuma maombi kujiunga na Chuo Kikuu cha serikali kuanguka katika udahili huo suala ambalo linaamanisha kuwa hakutakuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo Kikuu cha serikali.

Wachambuzi wa elimu nchini humo wanasema kuwa siku za wananfunzi kujiunga na Chuo Kikuu cha serikali kupitia mlango wa nyuma zimepita na kuanguka kwa wanafunzi hao kunaonesha wazi kuwa viwango vya kuingia Chuo Kikuu vimepanda.