NIGERIA

Kundi la Boko Haram lawauwa watu 20 katika jimbo la Borno nchini Nigeria

Kundi la Kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria limewaua wanachama 20 wa kundi la vijana linaloshirikiana na jeshi la serikali kupambana nao.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi linasema kuwa mauaji hayo yalitekelezwa kwa awamu tofauti na wanamgambo hao wa Boko Haram kuanzia Jumapili iliyopita katika jimbo la Borno.

Tangu mwaka 2009,  kundi hilo la Kiislamu lenye makao yake Kaskazini mwa nchi hiyo limekuwa likiisumbua serikali ya Nigeria kwa kutekeleza mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, kuvamia taasisi za serikali zikiwemo kambi za jeshi na kuyashambulia makanisa.

Mwezi Mei mwaka huu, rais Goodluck Jonathan alitangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Adawana na Yobe kutokana na kundi hilo linalopinga elimu ya Magharibi kuendelea kuhatarisha usalama wa kitaifa.

Jeshi la Nigeria limeanzisha msako mkali wa kuwasaka na kuwakamata wafuasi wa Boko Haram kwa kushirikiana na makundi ya vijana kutokana na ongezeko la mashambulizi ya kundi hilo ambalo limesababisha  zaidi ya watu elfu moja kuuawa na maelfu kujeruhiwa.

Serikali ya Marekani imeingilia kati juhudi za kuwasaka viongozi wa kundi hili ambalo pia limeathiri uwekezaji wa kiuchumi Kaskazini mwa nchi hiyo na inaahidi kutoa zawadi ya Dola Milioni 7 kwa yeyote atakayefanikisha kutoa habari za kumkamata kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau.

Wiki iliyopita, jeshi la Nigeria lilisema kuwa lilifanikiwa kumuua kiongozi wa kundi hilo kati ya mwezi wa Julai na mwezi wa Agosti madai ambayo kundi la Boko Haram halijazungumzia.

Juhudi za serikali ya Nigeria kuzungumza na viongozi wa kundi hili zimegonga mwamba.