SUDAN

Mapigano mapya yazuka katika jimbo la Blue Nile nchini Sudan

Mapigano mapya yamezuka kati ya jeshi la serikali ya Sudan na waasi katika jimbo la Blue Nile.

Matangazo ya kibiashara

Waasi wa SPLM-N wanasema kuwa walianza kukabiliana na jeshi la serikali katika wilaya ya Geissan karibu na mpaka wa Ethiopia na hadi sasa haijafahamika kama kuna watu waliopoteza maisha.

Mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yamekuwa yakiendelea kwa kipindi kirefu na kusababisha zaidi ya watu Milioni moja kukimbia makwao.

Serikali ya Khartoum imeendelea kuituhumu serikali ya Sudan Kusini kuwafadhili na kuwaunga mkono waasi kupambana na majeshi yake madai ambayo Juba inakanusha.

Kwingineko, mpatanishi wa mgogoro wa jimbo la Darfur nchini Sudan Mohamed Ibn Chambas amesema kuwa atawasilisha ripoti kwa serikali ya Khartoum kuhusu mazungumzo ya amani ambayo amekuwa akiyaongoza kati ya makundi pinzani ya waasi katika jimbo hilo.

Chambas amesema kuwa mazungumzo hayo yamekuwa yakifanyika mjini Arusha nchini Tanzania kati ya waasi wa Justice and Equality Movement (JEM) na wale wa Sudan Liberation Movement kundi  linaloongozwa na Minni Minnawi (SLM-MM) na juhudi zimepigwa kupata suluhu la kudumu .

Waasi hao wamekuwa wakishawishiwa na mpatanishi huyo kukubali kuketi katika meza moja ya mazungumzo chini ya mkataba wa amani wa Doha ili kuanza kwa mazungumzo kuhusu mzozo huo.

Mazungumzo kati ya makundi haya mawili yamefanyika miaka miwili baada ya kutiwa kwa mkataba huo wa amani kati ya makundi hayo ambayo kwa zaidi ya miaka kumi yameendelea kupigana na serikali ya Sudan.

Machafuko katika jimbo la Darfur yalianza mwaka 2003 baada ya waasi wa JEM na wale wa SLM/A kuchukua silaha na kuanza kukabiliana na majeshi ya serikali ya Sudan kwa madai kuwa serikali ya rais Omar Al Bashir ilikuwa inawabagua kwa sababu wao hawana asili ya kiarabu.

Serikali ya Sudan iliwahami waasi wa Janjaweed ambao walianza kuwasaka watu weusi katika jimbo hilo na kuwaua katika machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Rais Bashir Al Bashir anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa makosa ya mauaji ya maelfu ya watu na makosa mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu.