KENYA

Marais wa Kenya, Uganda na Rwanda wakutana Mombasa

Marais wa nchi za Kenya, Uganda na  Rwanda wanakutana mjini Mombasa nchini Kenya kushiriki katika kongamano la kuimarisha miundombinu kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na kongamano hilo, mwenyeji wa kikao hicho rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anazindua ujenzi wa eneo jipya la kupokea mizigo katika bandari ya Mombasa itakayorahihisha uhifadhi wa mizigo ya mataifa hayo yanayotumia bandari ya Mombasa.

Kongamano hili linafanyika baada ya kikao cha pamoja cha marais hao kilichofanyika mwezi Juni jijini Kampala Uganda, kuweka mikakati ya kujenga barabara na reli ya mizigo kuunganisha nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.

Mradi huu unatarajiwa kumalizika mwaka 2018 na kuunganisha miji ya Mombasa, Kampala, Kigali, Bunjumbura na Juba na utagharimu Dola Bilioni 3 nukta 5 na kufadhiliwa na mataifa hayo.

Viongozi hao pia watakutana tena mwezi Oktoba mwezi huu jijini Kigali Rwanda kuthathmini hatua zitakazokuwa zimepigwa baada ya kongamano la Mombasa.

Wachambuzi wa maswala ya biashara na siasa wanasema kuwa mradi huu ni muhimu kwa muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kurahihisha biashara kati ya mataifa hayo ili kuinua uchumi wa nchi hizo.

Hata hivyo, hatua ya Tanzania kuachwa nje ya mradi huo inazua maswali mengi ikiwa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yako pamoja katika miradi ya maendeleo.

Dar es salaam inasema haina tatizo na mataifa hayo kuendeleza miradi ya maendeleo mradi tu isiingilie mikataba wa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwaka uliopita, Tanzania na Kenya walifungua barabara mpya kati ya nchi hizo mbili kutoka Athi River hadi mjini Arusha.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajiwa kukutana mwezi Novemba mwaka huu kupokea mapendekezo kuhusu kuwepo kwa sarafu moja katika Jumuiya hiyo.