KENYA

Abiria 41 waangamia katika ajali ya barabarani nchini Kenya

Watu 41 wameuawa katika eneo la Ntulele nchini Kenya baada ya kutokea kwa ajali ya barabarani Alhamisi asubuhi, katika barabara ya kutoka jijini Nairobi  kwenda Narok na kuwaacha abiria wengine zaidi ya 30 na majeraha.

Matangazo ya kibiashara

Kamanda wa Trafiki nchini humo Samuel Kimaru amesema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo la abiria kukosa mwelekeo na dereva kushindwa kulithibiti alipojaribu kulisimamisha.

Walionusurika katika ajali hiyo wanasema kuwa idadi kubwa ya abiria walipoteza maisha kwa sababu iliwachukuwa muda mrefu waokoaji na maafisa wa polisi kufika katika eneo la ajali hiyo.

Hii ndio ajali mbaya zaidi ya barabarani kutokea nchini humo mwaka huu huku takwimu zikionesha kuwa zaidi ya watu 1,300 wamepoteza maisha kwa kipindi cha miezi saba kadhaa zilizopita.

Polisi nchini humo wanasema ajali zimeongezeka nchini humo kwa sababu ya tabia ya madereva kuendelea kuendesha magari kwa mwendo wa kasi na pia magari mengi kukosa vidhibiti mwendo.

Kenya inaingia katika rekodi ya kuwa mojawapo ya nchi inayorekodi idadi kubwa ya vifo vya barabarani kutokana na zaidi ya watu zaidi ya watu 3,000 kupoteza maisha kila mwaka.

Serikali ya Kenya imekuwa ikiwahusisha wananchi wake katika kampeni za kuhakikisha kuwa ajali za barabarani zinapungua kwa kuwashtaki kwa vyombo vya sheria madereva wanaoendesha magari kwa mwendo wa kasi na pia kutoa mafunzo kwa madereva, juhudi ambazo zinaonekana hazijafua dafu.