GHANA

Mahakama ya juu nchini Ghana yasema rais Mahama alishinda urais kihalali

Mahakama ya Juu nchini Ghana imesema kuwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka uliopita na kumpa ushindi rais John Dramani Mahama ulikuwa huru na haki na alishinda kwa haki. 

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umetolewa na Majaji tisa wakiongozwa na Jaji William Atuguba ambaye ameeleza kuwa kesi hiyo imetupiliwa mbali na madai ya upinzani kuwa kulikuwa na wizi wa kura hayana msingi.

Hata hivyo, kuna baadhi ya Majaji ambao walionekana kukiri kuwa kulikuwa na wizi wa kura lakini wengi wakapinga na hivyo kumpa ushindi rais Mahama.

Uamuzi huo umetolewa  baada ya kesi hiyo iliyowasilishwa na chama cha New Patriotic Party, kusikilizwa kwa miezi saba kupinga ushindi wa  Mahama wa asilimia 50 nukta 7 dhidi wa mpinzani wake Nana Akufo-Addo aliyepata asilimia 47 nukta 7.

Nana Akufo-Addo alifika Mahakamani kupinga matokeo hayo ambayo anasema hayakuwa ya kweli na kulikuwa na wizi mkubwa wa kura na rais Mahama hakushinda kwa haki madai ambayo chama cha rais Mahama cha NDCP kinapinga.

Maelfu ya maafisa wa polisi wanapinga kambi katika miji mbalimbali nchini humo hasa jijini Accra kukabiliana na hali yeyote ya uvunjifu wa amani ambayo inaweza ikatokea.

Vyama vyote vya kisiasa nchini humo vilisema kuwa vitakubali uamuzi wa Mahakama hiyo ya juu ili kuendeleza rekodi nzuri ya demokrasia nchini humo ambayo imeonekana kupigiwa mfano barani Afrika.