DRC

Mapigano yachacha Mashariki mwa DRC kati ya majeshi ya UN na waasi wa M 23

Mapigano mapya yamezuka Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya majeshi ya serikali yakisaidiwa na yale ya Umoja wa Mataifa dhidi ya waasi wa M 23 karibu na mji wa Goma.

Matangazo ya kibiashara

Wakaazi wa mji wa Goma wanasema wanasikia milipuko ya risasi mjini humo na watu hawatembei katika mji huo kama kawaida.

Mapigano haya mapya yanazuka siku moja baada ya mwanajeshi mmoja wa kulinda amani kuuliwa  na wengine watatu kujeruhiwa  katika makabiliano hayo.

Wiki hii, jeshi la serikali ya DRC likisaidiana na lile la Umoja wa Mataifa limekuwa likikabiliana na waasi wa M 23 katika eneo la Kibati karibu na mji wa Goma.

Kiongozi wa jeshi la kulinda amani MONUSCO Martin Kobler, amesema kuwa mwanajeshi aliyeuawa ni raia wa Tanzania na inaaminiwa alilengwa na kombora la waasi wa M 23 katika eneo la Kibati ambalo waasi hao wanasema ni ngome yao.

Aidha, Kobler ameongeza  kuwa mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo hauwezi kutatuliwa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi na badala yake mazungumzo ya amani ya Kampala yanastahili kurejelewa ili kupata suluhu la kisiasa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amedokeza kuwa, kwa mara ya kwanza jeshi la MONUSCO limetumia ndege zake za kivita kukabiliana na waasi wa M 23 ambao wameonekana kujihami kwa silaha nzito.

Waasi wa M 23 wakiongozwa na kiongozi wao Betrand Bissimwa wanalishtumu jeshi la serikali kwa kuanza kuwashambulia katika ngome zao madai yanayopingwa na jeshi kupitia msemaji wake Mashariki mwa nchi hiyo Olivier Hamuli anayesema wao ndio waliovamiwa.

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kinsasha na waasi wa M 23 yamegonga mwamba jijini Kampala Uganda suala ambalo limeendelea kuhatarisha usalama Mashariki mwa nchi hiyo.

Mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa ukiendelea kwa kipindi kirefu na ulizorota mwaka uliopita baada ya kuzuka kwa kundi la M23 lililodai kubaguliwa na serikali ya Kinsasha.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikituhumiwa na jirani zao DRC na Umoja wa Mataifa kufadhili na kuwaunga mkono waasi wa M 23 tuhma ambazo Kigali imeendelea kukanusha.

Jeshi la kulinda la umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini tayari liko Mashariki mwa nchi hiyo kukabiliana na makundi ya waasi.